WASHINGTON, MAREKANI
RAIS Donald Trump anatarajiwa kutangaza ushindi dhidi ya kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) katika hotuba yake ya hali ya Taifa.
Pia anatarajia kutoa wito wa matumaini, umoja na mshikamano katika hotuba hiyo, ambayo wenye shaka wanajiuliza iwapo anaweza kufanikiwa katika kushawishi mwanzo mpya baada ya miaka miwili ya mtengano wa kichama pamoja na mashambulio kwa baadhi ya watu.
Kabla ya hotuba yake jana, Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi alisema ana matumaini kusikia dhamira kutoka kwa Trump katika masuala yanayoungwa mkono na vyama vyote, kama vile kupunguza bei ya dawa na kujenga miundo mbinu nchini hapa.
Trump atazungumza katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mbele ya wajumbe wa seneti na wawakilishi pamoja na maafisa wengine wa serikali.
Wakati akitarajia kutangaza ushindi dhidi ya IS nchini Syria, maafisa wa jeshi la nchi hiyo wanaendelea kuhofia kuwa kundi hilo linavuta muda hadi pale Marekani itakapoondoka nchini humo.