BRUSSELS, UJERUMANI
RAIS wa Marekani, Donald Trump, ameanzisha mashambulizi dhidi ya biashara ya mauzo ya magari ya Ujerumani nchini Marekani, katika ishara ya hivi karibuni ya mzozo wa biashara katika kanda ya Atlantic.
Akizungumza baada ya vyombo vya habari vya Ujerumani kumripoti Rais wa Marekani akiwaelezea Wajerumani kuwa wabaya, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, alijaribu kupunguza uzito wa mgogoro huo wa karibuni zaidi tangu alipoingia madarakani, akitanguliza sera yake ya Marekani kwanza.
Akipendekeza kuwa matamshi yaliyoelekezwa kwa Trump yalikuwa yamepotoshwa, Juncker alithibitisha kwamba Trump alizungumzia ziada kubwa ya biashara ya Ujerumani na Marekani katika sekta ya magari wakati wa mazungumzo mjini Brussels siku ya Alhamisi.
Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyeuliza iwapo ni kweli Trump alisema Wajerumani ni wabaya, Juncker alisema katika mkutano wa G7 nchini Italia uliohudhuriwa na Trump na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kwamba suala hilo limetiwa chumvi.
"Sitaki kuzungumzia, lakini nalazimika kulizungumzia hili kwa sababu tulikuwa na mkutano na Rais Trump ambao ulikuwa wa kirafiki sana na wa manufaa. Siyo kweli kwamba rais alichukua msimamo wa kishari kuhusu ziada ya biashara ya Ujerumani. Nadhani kiukweli, na kwa mara ya kwanza ni kweli, kwamba huu ni mfumo halisi wa tafsiri."
Ujumbe ulifikishwa lakini si kwa ushari
Mshauri wa kiuchumi wa Trump, Gary Cohn, pia alisisitiza kuwa majibizano hayo yalikuwa ya kirafiki, lakini kwamba suala muhimu kwa utawala mpya wa Marekani lilikuwa limewekwa mezani. Cohn alieleza kuwa, Trump alisema Wajerumani ni wabaya kwenye biashara, lakini binafsi hana tatizo na Wajerumani.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ujerumani, Trump alilalamika vikali kuhusu kampuni mfano wa Volkswagen, BMW na Mercedes kuuza mamilioni ya magari nchini Marekani na kuapa kukomesha mauzo hayo. Bila kujali ukweli hasa ni upi, suala hilo halikuwazuia Trump na Merkel kufurahia wakati wao pamoja mwanzoni mwa mkutano wa G7, walipoonekana wakicheka wakiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk.
Wasaidizi wa Juncker walishutumiwa mwezi uliopita kwa kuvujisha maelezo ya mkutano wa chakula cha jioni alioufanya na May kuhusu Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya. Uvujishaji huo ulivifikia vyombo vya habari vya Ujerumani na kumlazimu Tusk kuonya kwamba, kukosekana kwa faragha kutayafanya mazungumzo ya Brexit kuwa magumu.
Wasiwasi miongoni mwa wanachama wa G7
Suala la magari ya Ujerumani lililipuka wakati wasiwasi umetanda miongoni mwa washirika wa Marekani katika kundi la G7, kwamba sera ya Trump ya Amerika Kwanza huenda ikasababisha hatua za kujihami ambazo zinaweza kurudisha nyuma miongo kadhaa ya uhuru wa kibiashara miongoni mwa mataifa yaliyoendelea zaidi duniani.
Wakati wa kampeni zake za uchaguzi, Trump alizituhumu China, Ujerumani na mataifa mengine kwa kuendesha ziada ya biashara na Marekani kwa kuharibu nafasi za ajira na maendelea ya Wamarekani wa kawaida kwa msaada wa sarafu zilizochezewa.
Tangu kuchaguliwa kwake, bado hajatekeleza hatua zozote muhimu za kujihami na Umoja wa Ulaya umeyatafsiri makubaliano ya kufungua biashara kati ya Washington na China, kama ishara kwamba unyumbulifu na utashi vina uwezekano mkubwa wa kuongoza sera ya biashara ya Marekani.