23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Trump awatisha wanaolaani kifo cha Mmarekani mweusi aliyeuawa mikononi mwa polisi

 WASHINGTON, MAREKANI 

RAIS Donald Trump wa Marekani amewaita ´vibaka´ waandamanaji mjini Minneapolis wanaolaani kifo cha mmarekani mweusi aliyekuwa chini ya mikono ya polisi. 

Rais Trump ambaye juzi Alhamisi alisema amehuzunishwa na kifo cha George Floyd, mwanaume mweusi aliyefariki dunia akiwa chini ya mikono ya polisi ametoa matamshi hayo ya kitisho baada ya waandamanaji wenye hasira kukichoma moto kituo cha polisi mjini Minneapolis. 

Akiandika kupitia ukurasa wa Twitter Trump amesema vurugu zinazoendelea zinafanywa na makundi ya vibaka na zinaharibu heshima anayostahili Floyd aliyefariki dunia siku ya Jumatatu baada ya kukandamizwa shingoni kwa kutumia goti na polisi mmoja mzungu. 

Kiongozi huyo aliyeuita mkasa wa Floyd kuwa wakusikitisha amesema tayari amezungumza kwa njia ya simu na Gavana Tim Walz wa Minnesota uliko mji wa Minneapolis na kumuarifu kuwa jeshi liko tayari na litachukua udhibiti pindi waandamanaji watakapoanza tena kufanya uharibifu wa mali. 

Trump ambaye mara nyingi amekuwa kimya linapokuja suala la ukatili wa watu weupe dhidi ya jamii ya wachache ya watu weusi nchini Marekani, amekosoa mwenendo wa polisi aliyesababisha kifo cha Floyd na kutoa wito wa haki kutendeka. 

UCHUNGUZI 

Tayari ofisi ya mwanasheria mkuu na idara ya upelelezi wa jinai mjini Minneapolis imesema inafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na kifo cha Floyd ikiwa ni pamoja na jinsi haki za kiraia za mwanaume huo zilivyohujumiwa. 

juzi waandamanaji wenye hasira walikichoma moto kituo cha polisi kilichotelekezwa wakati maandamano yaliyoingia siku ya tatu kulaani kifo cha Floyd yakigeuka vurugu na kuenea hadi mji jirani wa St.Paul. 

Msemaji wa polisi amethibitisha maofisa wa jeshi hilo kuondolewa kutoka kituo hicho kwa ajili ya ulinzi kabla ya baadaye kuvamiwa na makundi ya waandamaji na kukitia moto. 

Maandamano yalizuka siku ya Jumanne, siku moja baada ya kifo cha Floyd ambaye kupitia video iliyorekodiwa na mpita njia alionekana akiomba msaada kwa kusema anashindwa kupumua wakati polisi mweupe akimkandamiza shingoni kwa kutumia goti akiwa amefungwa pingu. 

Floyd ambaye hakuwa na silaha lakini akituhumiwa kutaka kutumia fedha bandia kwenye mgahawa mmoja, alichukuliwa na gari ya wagonjwa kutoka eneo la mkasa huo na baadaye kufariki dunia. Kifo Floyd kimeutikisa mji wa Minneapolis na kuzusha maandamano kwenye miji mingine kote nchini Marekani huku viongozi wa majimbo wakitoa wito kwa waandamanaji kuacha vurugu. 

juzi biashara kadhaa kwenye eneo hilo zililazimika kuwekewa ulinzi zaidi katika juhudi za kuzuia uporaji huku usafiri wa treni za katikati ya mji ukisitishwa kutoka na wasiwasi wa usalama. 

Maandamano ya kulaani kifo hicho yameripotiwa tangu mjini New York, Denver, Columbus na hata huko Kentucky. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles