WASHINGTON, MAREKANI
RAIS Donald Trump wa Marekani anataka kesi ya kushitakiwa bungeni ipelekwe katika baraza la Seneti kwa sababu huko utafanyika utaratibu mzuri na anatarajia mgombea wa kiti cha urais, Joe Biden, atakuwa miongoni mwa mashahidi.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani ya White House, Hogan Gidley, amesema kuwa Trump anataka kesi hiyo ifikishwe katika baraza la Seneti kwa sababu ni wazi kuwa ni baraza pekee la bunge la nchi hiyo analoweza kutarajia utaratibu wa haki na kuendeshwa mashitaka kwa mujibu wa sheria chini ya katiba ya nchi hiyo.
“Tunatarajia hatimaye kuwasikiliza mashahidi ambao walishuhudia, na huenda walishiriki katika rushwa, kama Adam Schiff, Joe Biden, Hunter Biden, na yule anayejulikana kama mfichuaji,” alisema Gidley akidokeza kuhusu mbunge wa baraza la wawakilishi ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ujasusi ya bunge, Adam Schiff, ambaye anaongoza uchunguzi wa Rais Trump kushitakiwa.
Msingi wa hayo yote ni taarifa zilizofichuliwa na maofisa usalama wawili kuhusiana na mawasiliano ya siri aliyofanya Trump na Rais wa Ukraine yenye nia ya kumwangamiza kisiasa mpinzani wake kuelekea uchaguzi wa 2020, Joe Biden.
Tayari maofisa kadhaa, wakiwamo wanadiplomasia wametoa ushahidi mbele ya baraza la usalama kuhusiana na madai hayo.