24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Trump asimulia jinsi Baghdadi alivyojiua

WASHINGTON, MAREKANI

RAIS Donald Trump wa Marekani ametangaza kuwa  kiongozi aliyekuwa akijificha wa kundi la Islamic State , Abu Bakr al Baghdad alijiuwa mwenyewe wakati wa uvamizi wa kikosi maalum cha Marekani nchini Syria.

Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia televisheni,Trump alitangaza kwamba gaidi huyo namba moja duniani amefariki wakati wa uvamizi hatari wa usiku kaskazini magharibi mwa Syria na vikosi maalum vya Marekani.

Marekani ilikuwa imetoa kitita cha dola milioni 25 kwa yeyote atakayewezesha kupatikana kwa taarifa kuhusu mahali alipo Abu bakr al Baghdadi.

Trump alisema kwamba ndege aina ya helikopta iliyokuwa ikisafirisha kikosi hicho maalum iliondoka kutoka eneo ambalo halikutajwa baada mwendo wa saa 11 siku ya Jumamosi, wakati yeye na viongozi wengine walikuwa wamekusanyika katika chumba cha Ikulu ya Whitehouse.

Aliongeza kuwa; ndege hizo zilisafiri kwa muda wa saa moja na dakika 10 kutoka maeneo tofauti, huku operesheni ya ardhini ikifanyika kwa muda wa saa mbili.

Maofisa waliviambia vyombo vya habari nchini Marekani kwamba mapema siku ya Jumapili nchini Syria, vikosi maalum vya Marekani vililenga eneo moja la kijiji cha Barisha mkoani Idlib takriban kilomita tano kusini mwa mpaka wa Uturuki.

Idlib ndio ngome ya mwisho ya upinzani dhidi ya Serikali ya Bashar al Asad.

Inatawaliwa na muungano wa wapiganaji wa Jihad ambao unakinzana na Kundi la Islamic State (IS), lakini mamia ya wapiganaji wa kundi hilo wanaaminika kupiga kambi katika eneo hilo.

UVAMIZI ULIVYOFANYIKA

Trump alisema vitengo vya ujasusi nchini Marekani vilimchunguza Baghdadi kwa wiki kadhaa kabla ya operesheni hiyo na kwamba walijua eneo hilo lilikuwa na mahandaki kadhaa, huku mengi yakiwa na mwisho wake.

Siku ya Jumamosi, Trump aliamrisha ujumbe uliohusisha kundi moja la wanajeshi maalum, ndege nane na meli nyingine nyingi.

Ndege hizo zilipaa juu ya anga ya Uturuki, mbali na maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya Syria pamoja na yale ya Urusi.

Kwa mujibu wa Trump Urusi ilishirikiana na kufungua anga yake kwa ajili ya operesheni hiyo ya Marekani licha ya kutoambiwa kile kilichokuwa kikijiri.

”Operesheni hiyo ya kuingia na kutoka ilikuwa hatari mno. Kulikuwa na wakati ambapo tungekabiliwa vilivyo,” alisema .

”Ndege zetu zilipaa chini chini lakini kwa mwendo wa kasi”.

Huku ndege hizo zikikaribia katika nyumba hiyo zilishambuliwa lakini Trump anasema mashambulizi hayo yalimalizwa haraka.

Mkazi mmoja wa Barisha anasema kwamba ndege hizo za Marekani zilishambulia nyumba mbili na kuiharibu kabisa moja

Mwanakiji mmoja kutoka eneo la Barisha aliambia BBC kulikuwa na mashambulizi kutoka kwenye helikopta hizo kwa zaidi ya dakika 30 kabla ya vikosi vya ardhini kuingia eneo hilo, akiongezea kwamba ndege hizo zilishambulia nyumba mbili na kuiharibu kabisa mojawapo.

Kulingana na Trump baada ya ndege hizo kutua , wanajeshi hao maalum walilipua mashimo katika kuta ya nyumba hizo ili kukwepa kuingia ndani kupitia mlango wa mbele uliowekwa mabomu na baadaye kuanza kuondoa vifusi.

Rais huyo alisema kwamba Baghdadi alifariki baada ya kutorokea katika handaki lililo na mwisho, akilia na kupiga kelele.

Inaelezwa kuwa watoto 11 waliondolewa katika nyumba hiyo bila kujeruhiwa, huku watu wakisalimu amri na wengine wakipigwa risasi.

”Aliyekuwa amesalia alikuwa Baghdadi pekee katika handaki pamoja na watoto watatu”, aliongeza Trump.

”Alifika mwisho wa handaki , huku mbwa wetu wakimfukuza . Alikuwa ameweka mabomu ya kutega katika nguo yake ya ndani na akajilipua na watoto hao watatu”.

”Mwili wake ulikatwakatwa na mlipuko huo huku handaki hilo likiuangukia” , aliongezea.

Picha na kanda za video kuhusu kilichotokea baada ya uvamizi huo wa Marekani zilionyesha vifusi vya jengo lililoharibiwa pamoja na gari lililoungua ikiwa na mashimo chungu nzima ya risasi.

Trump amesema kuwa matokeo ya vipimo vya mabaki ya mtu aliyejilipua katika handaki hilo yalionyesha kwamba alikuwa Baghdadi.

”Vipimo hivyo vilifanywa na wataalam waliosafiri na vikosi hivyo maalum na walikuwa na sampuli ya vinasaba vya Baghdadi”, aliongezea.

Kulingana na Trump, wataalam hao pia walibeba vipande vya mabaki ya mwili wake katika ndege hizo, ingawa hakuna uthibitisho huru kuhusu kifo cha Baghdadi.

Wafuasi wa IS wamekuwa wakionya kuhusu kuamini taarifa hizo zinazotolewa na Marekani.

Zaidi Trump alisema; hakuna mwanajeshi ama afisa hata mmoja wa Marekani aliyeuawa katika operesheni hiyo, huku akieleza jinsi idadi kubwa ya wapiganaji wa Baghdadi na washirika wao walivyouawa pamoja naye.

Trump alisema  ni mbwa tu  wa Marekani ndiye alijeruhiwa katika handaki hilo ambalo Baghdadi alifariki.

Chombo cha habari cha Jihadi mjini Idlib kimesema kwamba basi la raia lilishambuliwa

WAKE WA BAGHDADI

Trump pia amesema kuwa wake wawili wa Baghdadi walipatikana wakiwa wamevalia fulana za ndani zilizowekwa mabomu ingawa nao waliuawa.

Haijajulikani iwapo wafuasi wa IS ama watoto waliokamatwa walijeruhiwa.

wapiganaji hao kwa sasa wanazuiliwa huku watoto hao wakiwekwa chini ya usimamizi wa mtu ambaye hakutajwa.

KUJIFICHA BAGHDADI IDLIB

Mji wa Barisha upo mamia ya kilomita kutoka eneo la jangwa lililo mashambani katika mpaka wa Syria na Iraq ambapo Baghdadi aliaminika kujificha.

Trump alisema, Baghdadi alikuwa Idlib kwa kuwa alikuwa na lengo la kujenga upya jeshi lake la wapiganaji wa IS baada ya vikosi vya Kikurdi vinvyoongozwa na Marekani kuteka ngome zake za mwisho zilizosalia karibu na kijiji cha Baghuz kilicho mashariki mwa Syria mwezi Machi.

”Hiyo ndio sababu iliyomfanya kusalia katika eneo hilo”, rais huyo aliongezea “Hilo ndio eneo muhimu unapozungumzia kujenga upya kundi hilo”.

Anasema ripoti muhimu za kijasusi kuhusu mipango ya siku zijazo ya Baghdadi ilipatikana wakati wa shambulio hilo na kwamba Marekani itamsaka yeyote yule atakayemrithi.

”Tunawajua watakaomrithi. Na tayari tumeanza kuwaaangazia”.

HUYU NDIYE BAGHDADI

Alizaliwa mwaka 1971 katika eneo la Samarra nchini Iraq.

Akiwa angali mtoto alidaiwa kupenda sama kusoma Quran na kufuata sheria za kidini, akiwalaumu ndugu zake wasiofutwa vizuri dini ya Kiislamu.

Lakini ilikuwa wakati ambapo alikuwa anafuzu kupata Stashahada ya somo la Quran katika chuo kikuu cha Saddam Husein , ndio wakati alijihusisha na msimamo mkali wa kundi hilo.

Mwishoni wa mwaka 2000 alikuwa ameanzisha kundi linalofuata sunna na aliendelea hadi kushirikishwa na kundi la al-Qaeda nchini Iraq ambapo kundi la Islamic State lilibuniwa.

Tangu 2014 amesalia kimya kwa muda mrefu huku kukiwa na uvumi wa kifo chake ambao haukuthibitishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles