NEW YORK, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump, amemfagilia rapa mahiri, Kanye West na mkewe, Kim Kardashian kwa uchapakazi wao mzuri katika kusaidia jamii.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 72, aliwafagilia mastaa hao juzi baada ya kukutana nao kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa rais wakati wa chakula cha hisani.
“Kwa sasa tunafanya mambo makubwa na Kanye West, kusema ukweli msanii huyu ana nguvu,” Trump aliwaambia wageni waliohudhuria hafla hiyo ya chakula cha hisani.
“Hata mkewe Kim pia amekuwa akionyesha juhudi za ukweli kusaidia jamii zinazowazunguka,” alisema Trump wakati akiwamwagia sifa nyota hao.
Mapema mwaka huu, Kim (37) pia aliwahi kukutana binafsi na rais huyo White House, ambapo aliweza kumwombea msamaha mfungwa Alice Marie Johnson ambaye aliwekwa ndani kwa muda mrefu bila msamaha kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya na akafanikiwa kumchomoa kifungoni.