24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Trump akinzana na mshauri wake wa usalama

TOKYO, Japan

RAIS  wa Marekani, Donald Trump na mshauri wake wa usalama wa taifa, John Bolton, wameonekana kukinzana juu ya uzito wa tishio la Korea Kaskazini lililoko hivi sasa.

Hatua hiyo imekuja baada ya ujumbe wa Twitter alioutuma mwishoni mwa wiki  kutoka mjini hapa, ambapo Rais Trump alimjibu  Bolton ambaye siku moja iliyopita aliwaambia waandishi wa habari kuwa hakuna shaka kitendo cha Korea Kaskazini kujaribu kombora la balistika la masafa mafupi limevunja azimio la Umoja wa Mataifa.

Kauli ya Bolton ilikuwa ni ya kwanza kutolewa na ofisa wa Marekani akieleza kuwa kitendo cha Korea Kaskazini kurusha kombora ni kukiuka azimio la Umoja wa Mataifa.

“Korea Kaskazini ilifyatua baadhi ya silaha hizo ndogo ambazo zimewakera baadhi ya watu wangu na wengine, lakini sio mimi mwenyewe,” Trump alisema katika ujumbe wake wa twitter.

Lakini baadhi ya wachambuzi wanaeleza kuwa kurushwa kwa makombora hayo ni suala lenye kuleta wasiwasi.

“Ni dhahiri kuwa kurushwa kwa kombora kunakiuka vikwazo vilivyowekwa na UN, haijalishi ni la umbali gani.

“Ukweli ni kuwa majeshi ya Marekani na raia nchini Korea Kusini na Japan tayari wako katika umbali ambao makombora ya Korea Kaskazini yanaweza kuwafikia.

“Hivyo basi kukubali makombora ya masafa mafupi au ya kati kunaiweka Marekani hatarini, na hivyo hivyo washirika wetu Japan na Korea Kusini,”  alisema Kevin Maher.

“Ukweli ni kuwa liko tatizo hata iwapo lengo ni kuonyesha mahusiano binafsi na dikteta Kim Jong Un kuwa yataizuia Korea Kaskazini kuendeleza programu yake ya nyuklia na makombora,”aliongeza ofisa huyo.

Katika ujumbe wake wa Tweeter,Rais Trump alisema pia alitabasamu wakati Kim alipomwita Makamu wa Rais mstaafu Joe Biden ni mtu mwenye ufahamu mdogo.

Ujumbe wa awali wa Tweeter wa Rais ulikosea jina la mgombea kiti cha urais kwa tiketi ya Demokratic  lililosomeka “Bidan” na baadae likarekebishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles