WASHINGTON, MAREKANI
RAIS Donald Trump ameliambia gazeti la Uingereza la The Sunday Telegraph katika mkesha wa ziara yake mjini London, kuwa Uingereza inapaswa kuchukua uamuzi wa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya (EU) bila ya makubaliano na kukataa kulipa euro bilioni 45 kama fedha ya kujitoa.
Matamshi hayo ya kiongozi huyo wa Marekani yanakuja baada ya kuliambia gazeti la The Sun la Uingereza kwamba anafikiria kwamba waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson kuwa atakuwa waziri mkuu bora kuchukua nafasi ya Theresa May.
May ni Waziri Mkuu wa sasa, ambaye atajiuzulu rasmi kisheria ifikapo Juni 7 baada ya kushindwa kukamilisha hatua ya kujitoa EU, yaani Brexit kupitia Bunge la nchi hiyo.
Trump anaanza ziara ya siku tatu nchini Uingereza leo, ambapo atakutana na Malkia Elezabeth wa pili na kuwa na mazungumzo na May.