25.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

Trump ahamishia vilio vya chaguzi Afrika Marekani

RATIFA BARANYIKWA Na MASHIRIKA YA HABARI

TUMEZOEA kusikia habari za  malalamiko ya kura kuibiwa hasa katika nchi za Afrika.

Tumezoea sana kusikia vurugu za uchaguzi na kutokubali matokeo Afrika.

Kwa nchi kama Marekani ambayo imekuwa ikitambulika kama baba wa demokrasia habari hizi zilikuwa ni nadra.

Ni miaka minne iliyopita katika uchaguzi uliomwingiza tajiri, bilionea Donald Trump madarakani tuliambiwa Urusi ilimsaidia kuiba kura kwa njia ya mfumo na hivyo kufanikiwa kuingia Ikulu. 

Jambo hili lilileta seke seke kubwa, na liliumiza wengi waliokuwa wakiamini hakuna ushenzi wa kuiba kura Marekani.

Leo hii miaka minne baadae Trump yule yule aliyesemekana kuibiwa kura, japo yeye mwenyewe alikana naye sasa analalamika kuibiwa kura.

Hapa Tanzania mtu anayependa haki angeweza kusema; “Muoshwa huoshwa”.

Mtu mmoja ambaye tulikuwa tukifuatilia pamoja kwa njia ya televisheni matokeo ya uchaguzi wa Marekani, baada ya kusikiliza hoja za Trump akasema; “Huyu jamaa ni Mwafrika mwenye ngozi nyeupe anayeishi Marekani”.

Vyombo vya habari vya Marekani ambavyo vilikuwepo juzi Ikulu ya Marekani -White House kwa ajili ya kuripoti mkutano alioitisha Trump ambao aliutumia kutoa malalamiko hayo ya kuibiwa kura baadhi kikiwamo kituo cha CNN walikata matangazo yaliyokuwa yakirushwa moja kwa moja.

CNN na baadhi ya vyombo hivyo vya habari  vinasema vililazimika kufanya hivyo kwasababu hoja za Trump kuibiwa kura hazina ushahidi wowote.

Japo Trump sasa amekimbilia Mahakamani, uchaguzi utakapofika mwisho na walichoamua majaji tutaona kama hoja zake na hukumu zina mashiko.

Tayari katika matukio mawili tofauti ya uchaguzi huu, Mahakama Kuu ya Marekani imekataa kuingiliwa, kutokana na maombi ya Republican ya kugeuza uamuzi. 

Hilo ninaweza kusema ndicho kinachoonekana angalau kutofautisha Marekani na nchi nyingi za Afrika, ambako wapinzani wanaolalamika kwa ushahidi huishia kupuuzwa kwa maneno tu.

Zaidi hata mifumo yake ya haki haiaminiki kwa sababu ya katiba zake kuonekana kumpa mamlaka makubwa rais.

Kwa ujumla matokeo ya uchaguzi huu hadi yatakapokamilika tutaona na kusikia mengi kutoka kwa Trump, Biden na Wamarekani wenyewe tofauti na chaguzi zilizopita.

MFUMO WA UPIGAJI KURA, MATOKEO KUCHELEWA

Mfumo wa upigaji kura katika uchaguzi wa mwaka huu ulibadilika tofauti na chaguzi zilizopita ukiwamo ule uliompa ushindi Trump ambao ulidaiwa kuchezewa na mataifa ya nje.

Upigaji kura safari hii umefanyika pamoja na njia nyingine kwa njia ya posta.

Trump aliulalamikia mfumo huo akisema unachukua muda mrefu na akasisitiza kuwa ni hatari matokeo yake kuchezewa.

Upande wa Biden ambao walikuwa wakipigia chapuo mfumo huo walikuwa wanasema ni salama zaidi na walihamasisha watu wengi kuutumia.

Malalamiko ya Trump pamoja na hayo kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya mwisho  limekuwa gumzo kubwa duniani kote  na uchaguzi huu umeonekana kuwa tofauti na mingine iliyopita.

Zipo sababu zilizo nyuma ya kuchelewa kwa matokeo hayo ambazo ni idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura ambayo inakadiriwa kufikia milioni 158.

Kama ndivyo idadi hiyo inaweza kuufanya uchaguzi huu kuwa wenye wapiga kura wengi wanaostahili tangu mwaka 1900. 

The Washington Post limeandika hadi sasa kura za mapema tayari zimevunja rekodi ya miaka 60 na majimbo 31 yamevunja rekodi ya mwaka 1980 na hivyo kuufanya uchaguzi huu kuwa na mchuano wa mkali.

Ukiacha hilo upigaji kura kwa njia hiyo ya posta, pamoja na utaratibu wa uhesabuji uliojiwekea kila jimbo kutokana na maambukizi ya virusi vya corona ni sababu nyingine ya kuchelewa huko.

Kama nilivyosema mwanzo upigaji kura kwa njia ya posta umeonekana kuchukua muda mrefu ukiacha pia zoezi lenyewe la kuhesabu.

Kamishna wa tume ya uchaguzi ya shirikisho Ellen Weintraub,katika mazungumzo na kituo cha CNN  amesema; ni kawaida kwamba matokeo ya mwisho hayajulikani usiku wa uchaguzi,kama alivyosema. 

Amesema matokeo rasmi huja wiki kadhaa baadae. 

Kamishna huyo amesema jambo muhimu zaidi ni kwamba kura zote zinahesabiwa.

Kwa kura ambazo zimekwishahesabiwa hadi kufikia jana mpinzani wa Trump,ambaye alipata kuwa makamu wa rais katika serikali ya Barack Obama, Joe Biden ndiye anayeonekana kuongoza.

Biden mwenyewe  amezungumza na umma wa Wamarekani na kutaja tena vipaumbele vyake katika kipindi hiki akiashiria ushindi wa urais.

Pamoja na kusema zoezi la kuhesabu kura halijakamilika lakini Biden amesema hatua ya ushindi inayoashiria ndio inafungua njia ya zingatio la kukabiliana na janga la corona, ubaguzi na mabadiliko ya tabia nchi miongoni mwa mambo mengine. 

Biden ameyasema hayo wakati kukiwa na ishara ya ushindi katika majimbo muhimu, wakati kwa upande wa mpinzani wake akiendelea kulalamikia kuchezewa rafu, na kutaka majimbo hayo kusimamisha zoezi la kuhesabu kura. 

Hadi jana Jumamosi Biden alikuwa akihitaji kura sita za wajumbe wa majimbo ilikufikia 270 inayohitajika kumuingiza Ikulu.

Katika majimbo yaliyokuwa yamebaki  jimbo la Arizona  ambako asilimia 94 za kura  zilikuwa zimehesabiwa Biden alikuwa ana asalimia 49.9 na Trump asilimia 48.6. Pennsylavania ambako wapo katika asilimia 96 Trump ana asilimia 49.2 na Biden 49.5.  Georgia ambako hadi jana kura asilimia asilimia  99 zilikuwa zimehesabiwa Biden alikuwa na asilimia   49.5  na Trump,  49.4 North Carolina ambako pia kulikuwa kumehesabiwa kwa asilimia  98 na Trump kapata asilimia 50.0  Biden ikiwa  48.6, Nevada asilimia  93 Trump kapata  48.0  na Biden  49.8.

Tayari kwa upande wa Pennsylavania chama cha Republican kimeitaka Mahakama Kuu kuwasimamisha maofisa wa uchaguzi, kusimamisha kura ambazo ziliwasilisha katika maeneo ya kuhesabu kura baada ya kupita siku ya uchaguzi. 

Kiongozi mwenye dhamana na masuala ya nje wa jimbo hilo, alisema kwamba maofisa wote wa vituo vya kuhesabu kura katika jimbo hilo wameamrishwa kutimiza takwa hilo, ingawa kwa upande wa Republican wanasema hakujawa na uhakika wa jambo hilo kutelezwa na maofisa wote. 

Lakini kabla ya uchaguzi huo, mahakama ya kuu ya  Pennyslavania iliidhinisha kwamba kura zilizopigwa siku ya uchaguzi na zikafika katika maeneo ya vituo hata kama zitawasili vituoni ndani ya siku tatu.

Katika matukio mawili tofauti, Mahakama Kuu ya Marekani imekataa kuingiliwa, kufuata maombi ya Republican ya kugeuza uamuzi. 

Timu ya kampeni ya Donald Trump  ipo katika mchakato wa kushiriki makabiliano ya kisheria, lengo likiwa ni uhalali kuwasili baada ya uchaguzi kwa kura zilizopigwa katika jimbo la Pennyslavania. 

Takwa hilo la kisheria la Republican linahusu rundo la kura zilizopigwa kwa njia ya posta, kutoka upande wa Pennyslavania, ambalo linajumuisha mji wa pili kwa ukubwa wa Pittsburgh.

HOFU, SILAHA NJE NJE

Wafuasi wa Trump wanaonekana kutoridhishwa kabisa mwenendo mzima wa matokeo hayo.

Tangu mwanzo baadhi yao waliweka wazi na wapo walioonekana wakiweka vizuri silaha zao za moto kuonyesha wako tayari kwa mapambano yeyote iwapo Trump hatashinda.

Hilo limejidhihirisha tena jana ambapo watu wawili  wenye kujihami na silaha walitiwa mbaroni, karibu na eneo ambalo kura zinahesabiwa ambazo zinatahamua nani atakuwa rais wa taifa hilo kati ya Rais Donald Trump na Joe Biden.

 Kwa mujibu wa polisi waliotiwa mbaroni ni Joushua Macias mwenye umri wa miaka 42 na Antonia LaMotta mwenye umri wa miaka 51. 

Wote wanatajwa kutoka maeneo ya Virginia, na kwamba hawakuwa na kibali cha kubeba silaha hizo zilizokuwa zimesheheni risasi. 

Wote kwa pamoja wameswekwa rumande wakisubiri mashitaka yao.

Taarifa zinasema mmoja wa watuhumiwa hao ni mfuasi wa Trump  na kwamba kabla ya kukamatwa alisambaza picha katika ukurasa wake wa Facebook akiwa nje ya jengo la kuhesabu kura katika mji huo wa Philadelphia, akiwa amevaa fulana yenye picha ya Trump.

HASIRA ZA WATOTO WA TRUMP ZAFICHUA MAANDALIZI YA VIJANA KUJIPANGA 2024 

Kutokana na mwenendo huo wa matokeo, juzi Trump alianzisha tena mapambano yasiyo ya kawaida.

Trump aliwashambulia moja kwa moja wachangiaji wakubwa, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, taasisi za utafiti na Democratic kuwa nyuma ya matokeo ambayo ameyaita si sahihi.

Hatua  za kisheria alichochukua Truimp kupinga matokeo hayo imeendeleza mjadala wa vurugu zinazokumba shughuli ya kuhesabu kura.

Wakati huo huo watoto wawili wa kiume wa Rais Donald Trump wamewashutumu wanachama wa Republican kwa kutomuunga mkono rais anapokabiliwa na ushindani mkali kutetea mhula wa pili madarakani.

Mtoto mkubwa wa Trump, Don Jr alikosoa chama hicho kwa kuwa dhaifu. 

Ndugu yake Eric alionya: “Wapiga kura wetu hawatawahi kuwasahau mkijifanya wanyonge!”

Hatua hiyo inaasharia mgawanyiko ulioibuka kati ya washirika wa Trump ndani ya chama cha Republican.

Ushandani mkali umeshuhudiwa lakini mgombea wa Democratic Joe Biden anaonekana kuelekea kupata ushindi.

Trump ameapa kupinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani akitilia shaka shughuli ya kuhesabu kura inavyoendeshwa akidai kumekuwa na visa vingi vya udanganyifu.

Wanasiasa wa ngazi ya juu katika chama cha Republican seneta wa Utah, Mitt Romney na Gavana wa Maryland Larry Hogan wameonya hatua ya kuhujumu mchakato wa kidemokrasia.

Lakini Don Jr, ambaye anaaminiwa kuwa na ndoto ya kujiunga na siasa ameelekeza ghadhabu yake kwa wale walio na azma ya kuwania urais mwaka 2024.

Aliandika kwenye Twitter: “Hatua ya kutochukua hatua kwa wanasiasa wanaotaka tiketi ya 2024 ya Republican ‘ inashangaza sana .

“Wana nafasi ya kuonesha kutoridhishwa kwao na hali ilivyo na kupigania wanachokiamini lakini wanahofia kuangaziwa vibaya na vyombo vya habari. Msiwe na hofu @realDonaldTrump ataendelea kupambana na wao wakiangalia!”

Ujumbe huo wa Twitter hiyo ulikuwa unamjibu Mike Cernovich, mwanaharakati wa masuala ya wanaume na mfuasi wa Trump, ambaye alikuwa amemkosoa mjumbe maalum wa zamani wa rais katika Umoja wa Mataifa , Nikki Haley.

Anadhaniwa na wengi kwamba anapania kuingia Ikulu ya White House mwaka 2024.

Trump Jr aliendelea kuandika: “Republicans wamekuwa wanyonge kwa miongo kadhaa hali iliyotoa nafasi kwa wapinzani kufanya vitu hivi.”

Ndugu yake Eric, aliandika: “Sisi ni Warepublican! Tuna ubavu wa kukabiliana na udanganyifu. Wapiga kura wetu hawatawahi kusahau mlichokifanya!”

Ndugu hao wawili waliendelea mbele na kuwataja na kuwasifu wanachama wa Republican ambao wamejitokeza kumuunga mkono baba yao.

Wafuasi wengine wa Trump walimlenga moja kwa moja Haley. 

Matt Gaetz, mbunge wa Florida, aliandika : “Wakati baadhi yetu tunampigania Rais Trump… Nikki Haley anamuomboleza. inasikitisha!”

Katika miaka yake minne ya siasa, Trump amefanikiwa kutumia chama cha Republican kwa maslahi yake na kupata uungwaji mkono wa 90% kutoka kwa wanachama dhati wa Republican.

Ilani ya chama mwaka huu ilifutwa na kubadilishwa na ahadi ya “kuunga mkono ajenda ya kwanza ya rais Marekani”.

Mzozo kati ya familia ya Trump na usimamizi wa chama huenda ukaibua maswali kuhusu mkondo utakaochukuliwa na chama hicho baada ya Trump kuondoka, iwe ni mwaka 2020 au 2024.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,454FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles