25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 23, 2021

Trump adaiwa kuomba msaada China uchaguzi ujao

WASHINGTON, Marekani

RAIS wa Marekani, Donald Trump alijaribu kuomba msaada wa Rais wa China, Xi Jinping ili kushinda awamu ya pili ya urais, mshauri wake wa zamani  kuhusu usalama wa taifa, John Bolton ameeleza katika kitabu chake kipya.

Bolton alisema Rais Trump, aliitaka China kununua bidhaa za chakula kutoka kwa wakulima wa Marekani, kwa mujibu wa maelezo ya awali ya kitabu ambacho kimeanza kuchambuliwa na vyombo vya habari nchini Marekani.

Mwandishi wa kitabu pia anasema Rais Trump “alisalia kuwa mbumbumbu wa namna ya kuendesha Ikulu ya White House”.

Serikali ya Trump inajaribu kuzuia kitabu hicho kuingia sokoni.

Kitabu cha Bolton chenye kurasa 577 kiitwacho The Room Where It Happened (Chumba ambacho yalitokea), kinatarajiwa kuanza kuuzwa Juni 23, mwaka huu.

Hata hivyo, Jumatano usiku, Wizara ya Sheria ya Marekani, ilipeleka maombi ya dharura kwa jaji wa mahakama kuzuia uzinduzi wa kitabu hicho.

Mchapishaji wa kitabu hicho Kampuni ya Simon & Schuster, imeeleza: “Maombi ya leo ya Serikali hayana uzito na yamechochewa kisiasa.”

Imesema maelfu ya nakala za kitabu hicho tayari zimeshasambazwa sehemu mbalimbali ulimwenguni na pingamizi la Serikali halitafua dafu.

Kwa upande mwingine, Rais Trump alipiga simu katika runinga ya Fox News na kueleza kuwa: “Bolton amevunja sheria. Hizi ni taarifa za siri na hakupata kibali cha kuzitoa.”

“Alikuwa ni mtu ambaye amekwisha kabisa,” aliongeza Rais Trump. “Nilimpatia nafasi .”

Bolton ambaye anatajwa kuwa mfuasi wa sera za kimataifa za mabavu, alikuwa kiungo na Ikulu ya White House Aprili 2018 na kuondoka Septemba, mwaka jana.

 Bolton alitangaza aliamua kujiuzulu nafasi yake, lakini Rais Trump alisema alimfukuza kwa kuwa alikuwa anapingana naye vikali.

Madai ya Bolton ni kuwa mazungumzo hayo yalifanyika baina ya Rais Trump na Rais Xi wakati wa mkutano wa G20 jijini Osaka, Japan Juni, mwaka jana.

Rais wa China alilalamika kuwa wakosoaji nchini Marekani, walikuwa wanachochea vita baridi baina ya mataifa hayo mawili, bw Bolton anaeleza kwenye kitabu kama ilivyochapishwa kwenye gazeti la New York Times.

“Alisisitiza umuhimu wa wakulima na kuongezeka kwa manunuzi ya China ya magaharage ya soya na ngano kutakuwa na mchango wa matokeo ya uchaguzi.”

Baada ya rais Xi kukubali kufanya majadiliano ya manunuzi ya bidhaa za wakulima kuwa kipaumbele katika majadiliano ya kibiashara ya nchi hizo mbili, Trump akamsifu kuwa “kiongozi bora zaidi katika historia ya China.”

Mpinzani wa Rais Trump kutoka Chama cha Democrats Joe Biden, ameeleza kuhusu kitabu hicho kuwa: “Kama maelezo haya ni ya kweli, si tu kwamba ni jambo ambalo halikubaliki kimaadili, bali pia ni ukiukaji wa Donald Trump wa majukumu yake kwa Wamarekani.”

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,794FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles