29.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

TRUMP ADAIWA ALIJITUNGIA TAARIFA ILIYOSIFU AFYA YAKE

WASHINGTON, MAREKANI


ALIYEKUWA daktari wa Donald Trump amesema si yeye aliyeiandika taarifa iliyomweleza Rais huyo wakati alipokuwa mgombea urais wa Chama cha Republican kuwa alikuwa na ‘afya nzuri ajabu’, vyombo vya habari Marekani vimeripoti jana.

“Trump alitunga maelezo na kuamrisha kuandikwa kwa barua yote,” daktari huyo Harold Bornstein alikiambia kituo cha televisheni cha CNN juzi.

Ikulu ya Marekani, White House haikuzungumzia mapema tuhuma za daktari huyo.

Bornstein pia amesema maafisa wa serikali walifanya uvamizi katika ofisi zake Februari 2017 na kuondoa nyaraka zote zilizohusu afya ya Trump.

Katika mahojiano na CNN, Bornstein amesema barua hiyo ya 2015 iliyodokeza Trump angekuwa ‘mtu mwenye afya bora zaidi kuwahi kuchaguliwa kuwa rais’ haikuwa tathmini yake kitaalamu kuhusu hali yake ya kiafya.

“Niliitayarisha nilipokuwa nasongwa,” alisema Bornstein ambaye haijabainika sababu za kutoa tuhuma hizo sasa.

Barua hiyo ilikuwa na pamoja na mambo mengine tamko kuhusu nguvu za kimwili za Trump na ukakamavu wake, ambavyo vilielezwa kuwa ‘vya kipekee’.

Vipimo kuhusu shinikizo la damu yake na pia uchunguzi mwingine wa maabara vilielezwa kuwa ‘vya kushangaza kwa uzuri wake’ na kwamba alikuwa amepoteza uzito wa kilo saba katika kipindi cha mwaka mmoja.

Barua hiyo iliongeza Trump hakuwa na aina yoyote ya saratani na hajawahi kufanyiwa upasuaji wowote wa mwili.

Wiki kadhaa kabla ya taarifa kuhusu afya yake kutolewa mwaka huo, Trump alikuwa ameandika kwenye Twitter kuwa taarifa ya afya ya Bornstein ingeonesha hana kasoro.

“Nina bahati kubarikiwa vinasaba vizuri,” Trump, ambaye ndiye mtu aliyechaguliwa kuwa rais akiwa na umri mkubwa zaidi Marekani, aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook wakati huo.

Daktari huyo mwenye makao yake New York, anasema walinzi binafsi wa Trump walifika katika ofisi zake jijini humo wakiandamana na wanaume wengine wawili Februari 3, 2017.

“Walikaa hapa kwa dakika 25 au 30 hivi, walizua vurugu,” Bornstein aliambia NBC News, na kuongeza kuwa kisa hicho kilimfanya kujihisi kama aliyebakwa, kuwa na hofu na masikitiko na huzuni.”

Anasema nakala halisi, ambayo ndiyo pekee aliyokuwa nayo ya rekodi ya afya ya Trump, ikiwa ni pamoja na ripoti za uchunguzi wa maabara, vyote vilitwaliwa na walinzi hao.

Kisa hicho kilitokea muda mfupi baada ya gazeti la The New York Times kuchapisha taarifa ambayo Bornstein alisema alikuwa amependekezea Trump anywe dawa ya Propecia, ambayo ni ya kuzuia upara.

Afisa wa habari wa White House Sarah Sanders baadaye alisisitiza kisa hicho hakikuwa uvamizi bali tukio la kawaida la kitengo cha matibabu cha Ikulu kumiliki nyaraka zote za afya ya Rais wa Marekani.

Januari mwaka huu, Trump pia alifanyiwa uchunguzi wa kiafya ambao ulidumu saa tatu kuhusu afya yake ya kiakili.

Daktari wake Ikulu, Ronny Jackson alisema wakati huo kwamba: “Sina wasiwasi wowote kuhusu uwezo wake wa kufahamu, kufikiria na kuelewa mambo.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles