WASHINGTON, MAREKANI
WABUNGE wa Marekani wamesema wanafanya uchuguzi iwapo Rais Donald Trump anajaribu kuuza teknolojia nyeti ya nyuklia kwa Saudi Arabia, ili kuwafurahisha wafuasi wake wafanyabiashara, ambao watafaidika na mpango huo.
Bunge la Marekani tayari limeshafungua uchunguzi dhidi ya pendekezo la utawala wa Trump, la kutaka kujenga vituo kadhaa vya nyuklia nchini humo. Mbunge Elijah Cummings, Mwenyekiti wa Kamati ya Halmashauri ya Uangalizi na Mageuzi, ameitaka Ikulu ya Marekani kuwasilisha nyaraka za suala hilo.
Inasemekana kuwa kuna mkutano uliofanyika miezi miwili tu baada ya Trump kuingia madarakani kati ya mkwewe, Jared Kushner, na mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia , muda mchache kabla ya kutangazwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa taifa hilo.
Ripoti ya Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi imesema mshauri wa zamani wa usalama wa taifa Michael Flynn na wenzake wawili ndio waliopendekeza mpango huo.
Waliuwasilisha kwa Tom Barrack, mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe ya kuapishwa kwa rais, na muungano wa kampuni za Marekani yakiongozwa na makamanda wa kijeshi waliostaafu na viongozi wa zamani wa Ikulu ya Marekani.