Trump aambiwa afike kwenye kikao cha tuhuma zake au anyamaze kimya

0
656

WASHINGTON, MAREKANI

BUNGE la Congress nchini Marekani limemwalika Rais wa nchi hiyo, Donald Trump katika kikao chake kitakachosikiliza tuhuma zinazomkabili kiongozi huyo, Disemba 4 mwaka huu.

Mwenyekiti wa kamati ya Congress ya masula ya sheria kutoka chama cha Democratic, Jerrold Nadler alisema Trump anaweza kuhudhuria au ”akome kulalamika juu ya mchakato” huo.

Kama atahudhuria, rais ataweza kuwahoji mashahidi.

Kikao hicho kitakua ni hatua itakayowezesha kuanzishwa kwa hatua nyingine katika mashtaka , yanayomuhusisha na Ukraine chanzo chake ni simu ambayo rais Trump alimpigia rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Trump anashutumiwa kuwashinikiza viongozi wa Ukraine kumchunguza hasimu wake kisiasa Joe Biden.

Katika mawasiliano ya simu hiyo, Trump alimtaka Zelensky amchunguze Joe Biden, ambaye kwa sasa ndie mgombea aliye mstari wa mbele kuwania kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Democratic katika uchaguzi wa urais wa mwakani, na mtoto wake wa kiume Hunter Biden, ambaye awali alifanyia kazi kampuni ya nishati ya Ukraine Burisma.

Uchunguzi unataka kubaini ikiwa Trump alitumia tisho la kuzuwia msaada wa jeshi la Marekani kwa Ukraine ili kuifanya imchunguze Biden na mwanae.

Rais Trump amekana kufanya kosa lolote na ameutaja uchunguzi huo kuwa ni ” hila”.

Wiki iliyopita, Kamati ya masuala ya ujasusi ilikamilisha wiki mbili za kusikiliza, kufuatia wiki kadhaa za vikao vya faragha ambapo waliwahoji mashahidi.

Mwenyekiti wa kamati ya ujasusi, Adam Schiff, anayeongoza uchunguzi huo alisema kamati za masuala ya kigeni na intelijensia – sasa zinaifanyia kazi ripoti yao, ambayo itatolewa  Disemba 3, mwaka huu.

Jerrold Nadler alisema katika taarifa yake kwamba alikuwa amemuandikia Trump akimualika kuhudhuria kikao cha kusikiliza tuhuma dhidi yake mwezi ujao.

” Rais ana uamuzi wa kuchukua ,” Nadler alisema

“Anaweza kuchukua fursa ya kuwasilisha katika kikao cha tuhuma au aache kulalamika juu ya mchakato.

” Natumai kwamba atachagua kushiriki katika uchunguzi, moja kwa moja au kupitia baraza, kama walivyofanya marais wengine kabla yake.”

Katika barua yake kwa rais, Nadler alisema itakuwa ni fursa nzuri ya kujadili mashtaka kwa misingi ya kihistoria na kikatiba.

” Pia tutajadili juu ya ikiwa madai ya matendo yako yataliwezesha Bunge kutekeleza mamlaka yake ya kuidhinisha vipengele vya mashtaka,” aliongeza.

Kamati ya masuala ya sheria ya bunge inatarajiwa kuanza kuandika miswada ya tuhuma – ambazo ni mashtaka ya kufanya makosa dhidi ya rais- mapema Disemba.

Baada ya kura, bunge linalodhibitiwa na Democratic, kesi itaendeshwa katika Bunge la seneti linalodhibitiwa na Republican.

Kama Trump atapatikana na hatia kwa theluthi mbili ya wabunge- matokeo ambayo yanaonekana huenda kutopatikane- atakuwa ni rais wa kwanza wa Marekani kung’olewa madarakani kupitia mashtaka ya aina hii.

Ikulu ya White House na baadhi ya Warepublican wanataka kesi iendeshwe kwa wiki mbili tu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here