26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

TRL YAFUFUA RELI YA KASKAZINI MATAYARISHO KWENDA ZIWA NATRON

 

 

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

SERIKALI imeanza utekelezaji wa ukarabati wa reli kati ya Korogwe, Mkoa wa Tanga hadi Moshi Kilimanjaro, iliyositisha kutoa huduma zaidi ya miaka minane iliyopita.

Ukarabati huo unaotekelezwa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), unatarajiwa kukamilika Juni mwakani na kugharimu Sh bilioni 14.

Ukarabati huu unahusisha kutengeneza madaraja, ukarabati wa reli yenyewe na vituo vya treni ambavyo vimechakaa kutokana na kutotoa huduma kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa TRL, reli hiyo iliacha kupitisha treni 2009, hii inamaanisha ukanda huo umekosa huduma ya usafiri kwa miaka minane.

Hali hii kwa namna moja au nyingine ni wazi kuwa ilikwamisha shughuli mbalimbali ambazo zingeweza kufanyika endapo reli hiyo ingeendelea kutoa huduma kwa kipindi hicho.

Tafsiri ya haraka hapa ni kwamba malori yalichukua nafasi ya kusafirisha mizigo ambayo ilisababisha kuharibika kwa barabara ambapo zimejengwa maalumu kupitisha magari yenye uzito mdogo na wakati.

Taarifa kutoka Kitengo cha Habari cha Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), inasema lengo la kufufua reli ni kwa ajili ya kuendeleza huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria katika mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro.

Inaeleza kuwa pia itaongeza fursa mbalimbali ikiwamo ufanyaji biashara katika vituo mbalimbali itakapopita.

Kufufuliwa kwa reli hii ni hatua muhimu kwa sasa, licha ya kuwapo mpango wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa ‘Standard gauge’, bado uhitaji wa reli hii ya zamani ni muhimu kwa kuzingatia kuwa bado Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi wa reli mpya inayotumia umeme.

Kwa kuwa usafirishaji wa mizigo kwa kutumia treni ni salama na nafuu (rahisi kibei), ni wazi kuwa itapunguza gharama kubwa za usafirishaji ambazo wafanyabiashara wamekuwa wakiingia wanaposafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam na Tanga kwa kutumia malori kwenda mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Kuimarisha reli hii kutachechemua biashara katika maeneo mengi yanayopitiwa na reli hiyo hususan maeneo ya vituo vya reli, ambapo biashara ndogo za uchuuzi na vyakula zitaongezeka na kupunguza tatizo la ajira japo kwa uchache.

Kwa kuwa gharama za mizigo zitakuwa chini tofauti na sasa, wafanyabiashara wengi wataweza kuagiza mizigo kutoka Tanga na Dar es Salaam kwa kuzingatia kuwa reli hiyo huungana na reli ya kati inayotoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na mambo kuwa bora kama zamani ambapo kulikuwa na mtandao wa reli nchi nzima.

Kufufuliwa kwa reli hii kutachagiza na kuongeza utendaji wa Bandari ya Tanga ambayo imekuwa ikisuasua hasa kutokana na kufa kwa reli hiyo kwa kipindi kirefu. Bandari bila usafiri  wa reli kwenda bara huwa haina maana kubwa.

Ni wazi kuwa wafanyabiashara wa mikoa ya Kaskazini mwa nchi wataweza kutumia bandari hiyo kupokea mizigo kutoka ng’ambo kwa kuwa umbali kutoka bandarini hadi miji ya Arusha na Moshi ni karibu kuliko kutumia Bandari ya Dar es Salaam. Hivyo basi, kufanya nchi kujitegemea kwenye usafiri wake wa mizigo kupitia bandari zake zaidi ya ilivyo sasa.

Ikiwa wafanyabiashara hao watatumia bandari hiyo, ni wazi kuwa hata bei ya bidhaa kwa mtumiaji wa mwisho itapungua kutokana na kupungua kwa gharama za usafirishaji ambapo zitashuka kutokana na kupungua kwa umbali kati ya bandari na masoko.

Mkoa kwa Tanga umekuwa maarufu kwa kilimo cha matunda mbalimbali na mkonge, mazao ambayo yanaweza kutumika katika uzalishaji viwandani hususan wakati huu ambapo Serikali inahimiza uchumi wa viwanda kuelekea kipato cha kati.

Wakulima wa matunda wataweza kuuza kwa urahisi matunda yao kwa watu wenye viwanda ambao watakuwa na uhakika wa usafiri kutoka mashambani hadi kiwandani na kwa gharama nafuu, ikilinganishwa na sasa ambapo viwanda vingi vimekuwa vikilazimika kuagiza malighafi ya kutengenezea vinywaji baridi kutoka katika viwanda vya nje ya nchi hususan nchini Malaysia.

Kinachosababisha wafanyabiashara wengi kuagiza malighafi nje ya nchi kwa sababu ya gharama za usafirishaji wa matunda hayo kwenda viwandani kuwa juu na kukosekana kwa miundombinu ya uhakika kwenda maeneo yanakolimwa matunda.

Kwa kuwapo reli hiyo ni wazi kuwa wakulima wanaweza kuwa na kituo maalumu cha kukusanyia matunda yao, ambapo wamiliki wa viwanda watakuwa wakienda kununua matunda hayo na kuyasafirisha kwa urahisi.

Inategemewa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji Tanga au Simba Cement atafurahia hali hiyo, kwani amelalamika kwa muda mrefu na kilio chake kimesikilizwa na hivyo kuweza kuteka vilivyo soko la Mwanza.

Kwa kuwa maeneo yaliyopitiwa na reli hiyo inayofahamika zaidi kama reli ya Tanga ni yale yanayojengwa viwanda hususan yale ya Mkoa wa Pwani, ni wazi kuwa Kiwanda cha Twyford kinachotengeneza vigae au kile cha vinywaji baridi cha Sayona vitakuwa na fursa kubwa ya kusafirisha bidhaa zao kwa gharama nafuu kwenda katika masoko ya mikoa hiyo ya Kaskazini na bara  hadi Mwanza na Kigoma.

Hii itasaidia kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo ikilinganishwa na sasa ambapo wafanyabiashara hulazimika kuuza kwa bei kubwa ili kuendana na gharama halisi za usafirishaji wa mizigo kutoka Dar es Salaam kwa kutumia malori.

Profesa Gabagambi

Profesa Damian Gabagambi  wa Chuo Kikuu cha Sokoine, anasema ufufuaji wa reli hiyo ni suala jema na umechelewa  kwani ilipaswa kuwa imefanyiwa ukarabati mapema zaidi ili kuimarisha usafiri katika ukanda huo hivyo kuharakisha ukuaji wa uchumi.

Anasema ili nchi iendelee ni lazima kuwe na miundombinu ya kutosha na imara hususani miundombinu ya reli ambayo anasema inapaswa kupishana mithili ya mishipa ya damu mwilini.

“Mishipa ya damu inavyopishana kwa wingi inamaanisha kuwa utendaji kazi unakuwa rahisi, reli zinapopishana kwa wingi inasaidia usafirishaji kuwa rahisi, inatakiwa kupewa nguvu kubwa ili ikamilike, tunaweza tukaona kuwa ni ghali sana lakini baadaye tutaona faida zaidi hapo baadaye.

“Tukiwekeza kwenye reli tutakuza uchumi wetu haraka na barabara zetu zitadumu, haiwezekani unafikiria kukuza uchumi alafu unategemea malori kusafirisha mizigo,” anasema Profesa Gabagambi.

Pamoja na Taifa kuwa na watu wenye siha njema na elimu bora, maendeleo ya Taifa hupimwa kwa kuangalia upatikanaji wa usafiri kwa uhakika na wa haraka unaounganisha miji mbalimbali katika nchi husika.

Hivyo ni dhahiri kuwa Serikali imelitambua hilo ndiyo maana imeamua kutekeleza miradi mikubwa ya reli ikianza na ule wa reli ya kiwango cha kamataifa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza inayounganisha mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga hadi Mwanza, huku kipande kingine kikielekea Kigoma kuungana na nchi za Burundi na Rwanda.

Mradi mwingine ulio katika mpango wa kutekelezwa ni pamoja na ule wa reli ya Standard gauge kutoka Bandari ya Mtwara hadi katika Liganga na Mchuchuma ambako kunajengwa machimbo ya makaa ya mawe na kiwanda cha chuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles