Na ASHA BANI,
ASKARI Polisi wawili wa kikosi cha usalama barabarani, wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani, wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Trafiki hao waliuawa jana mchana wakiwa eneo la Bungu B wilayani humo.
Mmoja wa mashuhuda wa mauaji hayo, ambaye hakutaka kutaja jina, alisema wakati askari hao wanauawa, walikuwa watatu wamekaa kwenye ‘benchi’.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, askari hao walikuwa wanakagua magari yanayopita katika kizuizi kilichoko katika eneo hilo.
Alisema askari waliouawa ni wanaume na aliyenusurika ni mwanamke baada ya kukoswakoswa risasi aliyorushiwa.
Askari waliouawa walitajwa kuwa ni Sajenti Salim na PC Matola, huku aliyenusurika jina lake halikupatikana mara moja.
Kutokana na vifo hivyo, watu waliouawa katika mazingira ya kutatanisha wilayani humo wamefikia 40.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gulamu Kifu, alipotafutwa jana kuzungumzia mauaji hayo, simu yake iliita bila kupokewa.
Kamanda Polisi, Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyaga, amethibitisha kutokea tukio hilo.
Kutokana na vifo hivyo kutokea kwa nyakati tofauti, viongozi mbalimbali wa Serikali wamefika wilayani humo na Mkuranga kuzungumza na wananchi na kujua njia sahihi za kukomesha vitendo hivyo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro ni miongoni mwa viongozi waliofika katika maeneo hayo na kuzungumza na wananchi kwa nyakati tofauti.
Wakati askari hao wakiuawa, Rais Dk. John Magufuli alikuwa mkoani Pwani kwa ziara ya siku tatu akikagua shughuli za maendeleo na kufungua miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo, Rais Magufuli aliwataka wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kuwabaini wahalifu wanaojihusisha na vitendo hivyo vya mauaji.
Alisema hakuna mwekezaji atakayekwenda kuwekeza katika maeneo hayo wakati watu wanauana na kwamba wanaochelewesha maendeleo ya wilaya hizo ni wananchi wenyewe kwa sababu wanawajua wanaofanya vitendo hivyo.
“Serikali ya awamu ya tano si ya kuchezewa, moto wameshaanza kuupata, waache watanyooka, hawatapita na nasema hawapiti.
“Hakuna dini inayosema watu tuuane, tuendelee kuwaombea (wahalifu) waokoke na kujua damu ya mtu inatahmani kubwa,” alisema Dk. Magufuli.