21.1 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

TRA yaweka rekodi makusanyo Desemba

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imevunja rekodi kwa kukusanya Sh trilioni 1.987 kwa Desemba 2019, ikiwa ni kiasi kikubwa kuwahi kukusanywa katika mwaka mpya wa Serikali ulioanza Julai 2019. 

Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam juzi, Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Edwin Mhede alisema ni kweli kwamba kitaalamu, miezi tofauti hailingani moja kwa moja, lakini kwa makusanyo hayo ya Sh trilioni 1.987 kwa Desemba 2019, TRA imevunja rekodi yake yenyewe iliyoiandika Septemba 2019.

Alisema kwa ulinganifu wake pekee ni kuwa kama ilivyo Desemba 2019,  Septemba 2019 nao ulikuwa mwezi wa rekodi, kwa kukusanya Sh trilioni 1.7, iliyokuwa ni sawa na asilimia 97.20 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 1.817.

“Makusanyo haya ya mwezi Desemba 2019 ni sawa na ufanisi wa asilimia 100.2 kutokana na kuwa na lengo la kukusanya kiasi cha Sh trilioni 1.9 katika kipindi hicho ambayo ni ukuaji wa wastani wa asilimia 22 ikilinganishwa na makusanyo ya Sh trilioni 1.6 kwa mwezi Desemba 2018,” alisema Dk. Mhede. 

Alisema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2019/20 inayohusisha Oktoba, Novemba na Desemba, TRA ilifanikiwa kukusanya mapato ya Serikali ya Sh trilioni 4.9 sawa na ufanisi wa asilimia 97.4 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 5.100. 

Dk. Mhede alisema makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 19.78 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa robo ya pili ya mwaka 2018/19 ambapo mamlaka hiyo ilikusanya Sh trilioni 4.151 ikiwa ni sawa na ufanisi wa asilimia 87.5 kutokana na lengo la kukusanya mapato ya Sh trilioni 4.7 katika kipindi hicho. 

“Kwa upande wa makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi Oktoba 2019, mamlaka ilikusanya Sh trilioni 1.4 na mwezi Novemba 2019 mamlaka ilikusanya Sh trilioni 1.5, makusanyo ambayo yalikuwa ni sawa na ufanisi wa asilimia 93.9 na asilimia 97.5 kutokana na malengo ya kukusanya Sh trilioni 1.57 na Sh trilioni 1.53 kwa Oktoba na Novemba 2019 sawia,” alisema Dk. Mhede.

Alisema makusanyo hayo yanaonyesha ukuaji wa asilimia 14.40 na asilimia 23.31 ikilinganishwa na makusanyo ya Oktoba na Novemba 2018 kwa pamoja.

Dk. Mhede alisema kuwa makusanyo hayo ni mwendelezo wa kiashiria cha wazi kwamba walipakodi na Watanzania walio wengi wameendelea kuelewa, kukubali na kuitikia wito wa Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Dk. John Magufuli kwa maendeleo ya taifa.

Alisema kwa kuwa walipakodi wengi wameitikia kulipa kodi kwa mujibu wa sheria, ni vyema asiwepo mlipakodi ambaye atathubutu kubaki nyuma.

Alieleza kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kufuata matakwa ya sheria kwa hiyari na kuungana na kundi kubwa linalolipa kodi kwa hiyari na kwa wakati, kwa kusukumwa na dhamira zao.

Dk. Mhede alisema suala hilo si tu kuwa ni muhimu kukidhi mahitaji ya dhamira, bali pia kumekuwapo na baadhi ya mikakati ya makusudi iliyochochea kiasi hicho kikubwa cha ukusanyaji wa mapato, ambayo ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria kama zilivyo. 

“Pia mamlaka imeendelea kuziba mianya ya ukwepaji kodi kwa kuwashirikisha kikamilifu wale wale ambao wamekuwa wakibainika kukwepa kodi, usimamizi wa matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki, elimu kwa walipakodi na maboresho ya huduma kwa mlipakodi

“Aidha, tunaendelea kujiimarisha kiteknolojia kwa kujenga mifumo rafiki ya ukusanyaji kodi, na maboresho tunayoendelea kuyatekeleza ndani ya mamlaka ili kufanya kazi kama timu moja, yaani, ‘One TRA, One Big Family’ ili kupata mafanikio zaidi ya haya ya mwezi Desemba 2019.

“Kwa namna ya kipekee napenda kuwashukuru walipakodi wale waliolipa kodi ya Serikali na kusababisha Mamlaka kufikia malengo yake, Bunge, Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, taasisi za Maendeleo, na sekta binafsi kwa kuendelea kuipatia ushirikiano stahiki katika kutekeleza majukumu yake ya kukadiria, kukusanya, na kuhasibu mapato ya Serikali,” alisema. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,592FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles