CHRISTINA GAULUHANGA NA PATRICIA KIMELEMETA
MAMLAKA ya Mapato Taanzania (TRA), imetoa siri ya vijana zaidi ya 29,000 kuitwa kwenye usaili wa nafasi 400 za kazi zilizotangazwa na mamlaka hiyo kati ya 56,000 walioomba.
Licha ya TRA kuhitaji wenye sifa za kuanzia shahada ya kwanza, waliomba hata wenye astashahada na hiyo ni moja ya sababu ya watu 29,324 kuitwa kwenye usaili wa kwanza.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa TRA, Gerald Mwanilwa, akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, alisema katika awamu ya pili ya usaili inayotarajiwa kufanyika Septemba 18, watakaoitwa ni 1,200 pekee.
Akitoa siri ya watu wengi kuitwa kwenye usaili wakati nafasi zikiwa chache, alisema lengo la TRA ni kuhakikisha wanapata vijana wenye sifa, watakaoweza kuajiriwa mahali popote kukusanya kodi kulingana na elimu waliyonayo.
“Lengo la TRA ni kupata vijana 400 ambao tutaweza kuwaajiri na kuwasambaza kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ili waweze kufanya shughuli za kukusanya kodi, hatua hiyo itaisaidia Serikali kupata mapato,” alisema Mwanilwa.
Alisema mamlaka hiyo inahitaji vijana wenye weledi, watakaotumia taaluma zao kwa masilahi ya taifa ili kupunguza mianya ya rushwa katika sekta ya kodi.
“Awali, kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakidai kuwa ajira za Serikali ni za kujuana.
“Hilo limechangia Serikali kuunda mfumo mpya wa kusimamia ajira chini ya Sekretarieti ya Ajira, tunaamini vijana watakaobahatika kupata ajira TRA ni wale wenye sifa stahiki,” alisema.
Mwanilwa alisema katika mchakato wa awali, sekretarieti hiyo iliunda kanda maalumu kusimamia usaili wa vijana hao katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Alisema kanda hizo ni Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Tanga, Mwanza, Tabora, Kagera, Arusha, Mtwara na Dar es Salaam ambapo kulikua na vituo viwili ya usaili, kimoja kikiwa kwenye Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni.
Mwanilwa alisema maombi yaliyowasilishwa kwa mara ya kwanza yalikuwa ya vijana 56,000 kati yao kulikuwa na watumishi wa idara nyingine za Serikali, wanafunzi na wasio na ajira.
Alisema katika kundi hilo kulikuwa na vijana wenye elimu ya astashahada, stashahada na ya juu, wakati TRA ilikuwa inahitaji vijana wenye elimu ya juu kuanzia ngazi ya shahada.
Mwanilwa alisema kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo ililazimika kuwachuja na kupata vijana 29,324 waliofanya usaili wiki iliyopita.