24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YATOA ELIMU MABADILIKO YA KODI

Na KOKU DAVID


KATIKA kuhakikisha elimu ya kodi inamfikia kila mdau wa kodi nchini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana na wadau wa kodi kwa lengo la kuwafundisha mabadiliko mbalimbali katika kodi.

Hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano uliopo Benki Kuu (BOT) jijini Dar es Salaam, TRA ilikutana na viongozi na watumishi kutoka idara na taasisi mbalimbali katika semina ya siku moja ili kuwafundisha mabadiliko katika sheria mbalimbali za kodi kupitia sheria ya fedha ya kila mwaka husika.

Pamoja na kuwapa elimu, pia semina hiyo ilikuwa na lengo la kubadilishana mawazo, uzoefu pamoja na changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Katika utendaji wake wa kazi, mamlaka hiyo imekuwa ikikutana na changamoto mbalimbali kutoka kwa wadau wa kodi ambazo hivi sasa mpango mkakati uliopo ni kuhakikisha wanaziondoa kabisa.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kutumia mashine za kielektroniki za kodi (EFDs) kwa lengo la kukwepa kulipa kodi stahiki, ikiwa ni pamoja na biashara za magendo zinazoingizwa nchini kwa njia ambazo si rasmi.

Hata hivyo, mamlaka hiyo imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha inawakamata wafanyabiashara hao wanaofanya biashara hizo za magendo, ikiwa ni pamoja na kutaifisha mizigo yao ili kukomesha biashara hizo.

Kwa upande wa mabadiliko ya sheria za kodi, utekelezaji wake unatokana na uelewa wa pande mbili ambazo ni mkusanyaji wa kodi pamoja na mlipaji wa kodi.

Pande hizi kila mmoja ana wajibu wa kuzijua na kuzielewa ili kuweza kurahisisha utendaji kazi wa maofisa wa TRA, lakini pia wa walipa kodi kulipa kodi iliyo sahihi na kuiwezesha Serikali kupata kodi yake.

Kwa kutambua umuhimu wa elimu ya kodi, semina waliyoiandaa ililenga kupitia maeneo muhimu ya mabadilko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 pamoja na Kodi ya Zuio kutoka kwa wakandarasi na wazabuni wa miradi mbalimbali pamoja na huduma.

Pia, kupitia semina hiyo wadau hao walipata elimu kuhusiana na matumizi ya mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kutumia mashine za kieletroniki za kodi (EFDs).

Kamishna wa Idara ya Walipakodi wakubwa, Neema Mrema, anasema TRA inatambua ushirikiano inaoupata kutoka kwa taasisi za Serikali na mashirika mbalimbali ya umma katika kutimiza azma ya kufikia uchumi wa kati.

Anasema azma ya uchumi wa kati itafikiwa iwapo kila mmoja atatekeleza majukumu yake kikamilifu, hivyo ushirikiano endelevu unahitajika ili TRA iweze kukusanya mapato sahihi na kwa wakati na kuweza kutimiza kile kinachokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mamlaka hiyo ya Mapato imefanya maboresho mbalimbali yenye lengo la kuongeza weledi na ufanisi katika ukusanyaji mapato, utoaji huduma na usimamizi mzima wa sheria na mifumo ya kodi.

Lengo la juhudi  hizo ni kuhakikisha mapato ya Serikali yanaongezeka, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kufanya mambo ya maendeleo kwa wananchi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles