Nyendo Mohamed
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, wamefanikiwa kukamata vipuri ambavyo kama vingeingizwa nchini na kuunganishwa, vingeweza kutengeneza mashine 500 za michezo ya kubashiri ambayo ingekwepa kodi ya zaidi ya Sh milioni 600 kwa mwaka.
Mashine hizo zimekamatwa katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam zikiwa zimeagizwa bila kufuata taratibu za uagizaji wa vifaa vya aina hiyo na raia wa China Wu Dingfeng (31), mwajiriwa wa kampuni ya Bonanza Trade.
Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Kikodi Ilala Steven Kauzen, alisema Agosti 26 walitoa taarifa ya kuingizwa mashine hizo kupitia uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ambazo zilikuwa zinaelekea mkoa wa Kilimanjaro ambako zilitarajiwa kupokewa na. Dingfeng.
Alisema TRA kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi Mkoa wa Kilimanjaro waliendelea kufanya uchunguzi ambapo walimkakata Dingfeng na kumfungulia mashitaka.
Meneja huyo alisema kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo ni matokeo ya operesheni inayoendelea kati ya TRA, Bodi ya Michezo ya kubahatisha na vyombo vya ulinzi ili kubaini wanaofanya biashara hiyo bila kufuata taratibu za usajili mashine na biashara hizo.
Alisema pia wamepata taarifa ya uwepo wa mashine 10,000 ambazo hazijasajiliwa, jambo ambalo ni kinyume na taratibu na linachangia kupunguza mapato ya Serikali.
“Kwa taarifa ambazo nimepatiwa ni kwamba mashine nyingi zinaingia kupitia kanda ya kaskazini, nyanda za juu kusini na kanda ya ziwa zikitoka nchi jirani ambazo nyingi kati ya hizo zimekuwa zikiingizwa kwa njia za panya bila kusajiliwa na bodi ya michezo ya kubahatisha”, alisema Kauzen.
Kwa upande wake Meneja wa TRA upande wa Forodha (JNIA), Wilson Kantambula, alisema kutokana na kubaini mbinu mbalimbali wanazotumia watu hao tayari wameweka taratibu ikiwemo kupatiwa elimu ya kutosha kwa maofisa namna ya kuwabaini wale wote waanaokinzana na taratibu hizo.
“Hata hivyo, tayari tuna mfumo mzuri ambao unatusaidia kubaini wale wote wanaojaribu kupitisha mashine hizo bila kuwa na kibali kutoka bodi ya michezo ya kubahatisha” alibainisha Kantambula