26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YATAKA TAASISI ZA SERIKALI KULIPA KODI  VAT

Na KOKU DAVID



MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezitaka Taasisi zote za Serikali ambazo zinafanya biashara na kuingiza mapato zaidi ya milioni 100 kwenye biashara hizo kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani kama serikali ilivyoagiza.


Kupitia Waziri wa Fedha serikali ilizitaka taasisi hizo kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) ili kuisaidia kuweza kupata mapato yake stahiki kwa mujibu wa sheria.


Sambamba na matumizi ya mashine za EFDs, taasisi hizo zilitakiwa kujitokeza ili ziingizwe kwenye mfumo wa kulipa kodi badala ya kusubiri kufuatwa na maofisa wa TRA.


Mfano wa taasisi hizo zilizotakiwa kujitokeza ili ziingizwe kwenye mfumo wa ulipaji wa kodi ni kama Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Suma JKT pamoja na taasisi nyingine zote za serikali.


Pia ili kuhakikisha kila mwenye mapato analipa kodi kulingana na sheria inavyowataka, mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kukusanya Kodi ya Ongezeko la Thamani kutoka kwa makampuni ya utalii.


Kutokana na kuziba mianya mbalimbali ya upotevu wa mapato, mamlaka hiyo imekuwa ikikusanya mapato hadi kuvuka lengo.
Kwa mwaka huu wa fedha ambao unaelekea ukingoni, mamlaka hiyo inatarajia kukusanya kiasi cha sh trilioni 15.1 ya lengo ambalo serikali imeitaka kukusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali zikiwemo taasisi za serikali. 
Mafanikio hayo ya ukusanyaji mapato ndani ya TRA yanatokana na utekelezaji wa mikakati yake ya kuhakikisha mapato yanaongezeka hadi kuvuka lengo.


Pamoja na changamoto mbalimbali lakini baada ya kuziba mianya ya upotevu wa mapato mamlaka hiyo ilifanikiwa kuongeza ukusanyaji mapato kwa kiwango cha juu ikilinganishwa na miaka iliyopita.


Sambamba na  uzibaji wa mianya ya upotevu wa mapato, mamlaka hiyo imeimarisha mifumo yake ikiwa ni pamoja na kuongeza wataalamu ambao watasaidia kutatua changamoto hasa katika matumizi ya mashine za EFDs.


Pia mamlaka hiyo iligawa mashine za EFDs kwa wafanyabiashara mbalimbali na kwamba lengo lilikuwa ni kugawa mashine 5703 kama moja ya mikakati ya TRA ya kuziba mianya ya upotevu wa mapato lakini pia kuwasaidia wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara zao kwa urahisi.


Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo anasema kuwa hivi sasa matumizi ya mashine za EFDs hayaepukiki hivyo mamlaka imeimarisha mifumo yake ili kuweza kuondoa changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza.


Anasema kwa upande wa forodha pekee kwa mwaka wa fedha wa 2016/17, TRA ilijiwekea lengo la kukusanya sh trilioni 6.2 hivyo wafanyabiashara waliozoea kutumia njia za magendo wametakiwa kuacha kutokana na kuwa sheria kali zitachukuliwa dhidi yao iwapo watabainika.


Anasema mamlaka imesharahisisha mfumo wa uondoshaji wa mizigo bandarini (TANCIS) na kwamba mizigo haikai kwa muda mrefu kama ilivyokuwa hapo awali.


Pia mkakati mwingine ambao uliwekwa ili kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei, TRA iliendesha zoezi la uhakiki wa Namba za Utambulisho (TIN) kwa wafanyabiashara wote ikiwa ni pamoja na kutembelea maduka yote kukagua yanatumia mashine za EFDs.


Mamlaka hiyo imejiwekea utaratibu wa kutembelea maduka, nyumba pamoja na mitaa ili kuhakikisha wanakusanya mapato stahiki kutoka kwa kila anayestahili kulipa kodi ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles