TRA YAKUSANYA TRILIONI 14.4

0
485

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka wazi makusanyo yake ya fedha kwa kipindi cha mwaka 2016/17 kwa kufanikiwa kukusanya Sh trilioni 14.4.

Licha ya makusanyo hayo, sura ya bajeti ilionyesha kuwa jumla ya Sh trilioni 29.54 zilitarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho.

Bajeti hiyo ilitarajiwa kuwa na ongezeko la jumla ya Sh trilioni 7.04 103 ambazo ni sawa na asilimia 31.1, ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2015/16 ya Sh trilioni 22.49.

Ilielezwa kuwa makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.67 la makusanyo ya mwaka wa fedha wa 2015/16 ambao walikusanya Sh trilioni 13.3.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema makusanyo hayo yametokana na mikakati iliyowekwa na mamlaka hiyo.

Alisema katika makusanyo ya Juni, mamlaka hiyo ilikusanya Sh trilioni 1.37 huku Mei wakifanikiwa kukusanya trilioni 1.12.

“TRA imeendelea vizuri katika suala la ukusanyaji wa mapato na kwamba kila mwezi haijawahi kushuka chini ya Sh trilioni moja katika kukusanya mapato hali iliyotokana na mikakati mizuri ambayo imewekwa na mamlaka,” alisema Kayombo.

Alisema katika kuhakikisha mapato yanaongezeka, TRA imewataka wananchi wanaopata huduma kutoka kwa wafanyabiashara kudai risiti na wafanyabiashara kutoa risiti zinazotokana na mashine za kodi za EFD ili kuepuka kupata adhabu.

Kayombo alisema wamebaini mbinu za ukwepaji kodi zinazofanywa na wafanyabiashara ambao si wazalendo wanaowapa wateja risiti ambazo si za siku hiyo au ambazo haziendani na gharama halisi ya bidhaa iliyonunuliwa na kwamba TRA imejipanga kuhakikisha inawachukulia hatua watakaokamatwa.

Akizungumzia suala la ulipaji wa kodi ya majengo, Kayombo alisema wale wote ambao nyumba zao zimewekewa alama kubomolewa, hazitakiwi kulipia.

Alisema hivi sasa zimebaki siku tatu na kwamba wale wote ambao bado hawajalipia kodi za majengo, wanatakiwa kujitokeza ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here