27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yafuta minada ya hadhara, sasa kufanyika kwa mtandao

ASHA BANI-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetangaza kusitisha uuzaji wa bidhaa mbalimbali kwa minada ya hadhara kupitia kampuni za udalali na badala yake sasa itaendeshwa kwa njia ya mtandao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishana Mkuu wa TRA, Dk. Edwin Mhede, ambapo alitangaza kusitishwa kwa minada ya hadhara kwa ajili ya kuuza bidhaa mbalimbali kwa kutumia madalali.

Alisema kwa utaratibu mpya wa sasa minada hiyo itafanyika  kwa kutumia njia ya mtandao wa kielektroniki kwa kutumia tovuti ya TRA ambayo ni www.tra.go.tz ambao utaendeshwa kwa muda maalumu na kuonekana kwenye mfumo wa taarifa na kisha mshindi atatangazwa.

Alisema utaratibu wa minada kwa njia za madalali ulikuwa ukitumiwa katika uuzaji wa bidhaa mbalimbali za forodha ambayo ilikuwa ikiendeshwa na dalali aliyepewa kandarasi  na TRA kufanya minada hiyo.

Alisema wakati walikuwa wakitumia madalali kumeonekana kutokea na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja  na kufanyika mara moja kwa wiki hivyo  kwa kiasi kikubwa bidhaa haziuzwi kwa wakati na kupelekea serikali kutokomboa kodi kwa wakati.

Alisema changamoto nyingine ni washiriki wa mnada wamekuwa ni walewale kwa kujirudia na wengi wao kutokua wanunuzi na mara kadhaa wamekuwa wakiingilia minada na kusababisha kuharibu na kufanya wanunuzi wenye nia kushindwa kununua bidhaa hizo.

“Pia kumekuwa na vitendo vya kuzuia wengine na kupanga bei ambayo ni kinyume na busara ya misingi ya uchumi. Baadhi ya watu wenye hila waliweka mtandao wao,” Dk. Mhede.

Pia alisema kumekuwa na tuhuma na vitendo vya rushwa vikiwahusisha hata baadhi ya maofisa wa TRA na kukwamisha kufanyika kwa ufanisi.

“Ulipaji wa malipo ya awali ya asilimia 25 kwa washindi umekuwa ukihitaji washiriki kwenda eneo la mnada na fedha taslimu na kwa wale wanaolipa kwenye akaunti zao inawalazimu wawe na akaunti ya benki iliyopo kwenye eneo la mnada jambo ambalo ni hatari pia.

“Kumekuwa na mrundikano wa bidhaa zilizopitisha muda kwenye maeneo mbalimbali yaliyopo chini ya forodha bila kuuzwa jambo ambalo limekuwa likiathiri operesheni na kushindwa kutoa bidhaa  zingine zinazoingia au kutoka nchini kwa wakati,” alisema Dk. Mhede.

Alisema changamoto nyingine ni gharama zinazotumiwa na mamlaka kuendesha minada hiyo mikubwa na hivyo kazi kufanywa bila kuwa na tija.

Kutokana na changamoto hizo mamlaka ilisitisha minada hiyo ya hadhara kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja lakini kwa sasa imerudi ila itafanyika kwa njia hiyo ya mtandao.

Alisema pia uamuzi wa kusitisha minada ya hadhara ilikuwa ni kutokana na utekelezaji wa mpango kabambe wa serikali ya awamu ya tano wa serikali kuwa na serikali mtandao.ambapo wizara , idara, wakala na taasisi za serikali zinatakiwa kuendesha shughuli zake hasa za ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.

Alisema hata hivyo kuanzia Desemba 24, mwaka huu uhamasishaji utaanza kufanyika kwa njia ya mtandao ili wananchi wafahamu utaratibu huo mpya.

Dk. Mhede, aliongeza kuwa kwa kutumia mfumo huo TRA inatarajia kupata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na bidhaa nyingi kuuzwa kwa wingi kwa wakati na ushindani ulio wa haki kwa wateja na hatimaye makusanyo kodi kuongezeka.

Alisema watanzania wengi kupata fursa ya kununua bidhaa bila kuongeza gharama za kutumia madalali, sambamba na wanunuzi kuwa na muda wa kutosha wa kununua bidhaa na kutakuwa na ushindani wa haki.

“Mshindi atapata bili yake ya malipo ya awali ya asilimia 25 na malipo ya kumalizia ya asilimia 75 kwa wakati ili kulipia kodi kupitia mtandao na  atakwenda kulipia benki kupitia akaunti yake.

“Hivyo atalazimika kurudi tena TRA wakati wa kuchukua mzigo wake pia  mnunuzi atakua na uwezo  wa kulipia bili zote mbili yaani 25 asilimia na 75 kwa pamoja na kukamilisha malipo na kwenda kuchukua mzigo,” alisema Dk .Mhede.

Alisema pia mfumo huo wa kufanya mnada mtandaoni umeunganishwa na mfumo wa usajili wa magari kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa kadi za usajili kwa washindi watakaonunua magari .

Alisema mnada wa kwanza utafanyika Januari 2, mwaka 2020 kwa njia ya mtandao ambapo washiriki watapewa fursa ya kushiriki kwa siku kadhaa kabla ya mshindi kutangazwa na taarifa zote kuonekana kwenye mfumo.

Dk. Mhede alitoa utaratibu wa mnada na manunuzi kwamba mteja atatakiwa awe na kifaa chochote chenye mtandao popote alipo ikiwa ni pamoja na simu ya mkononi, kompyuta au kompyuta mpakato.

Pia atatakiwa awe amesajili kwenye mfumo  na kwa wale wasio na TIN watafanya usajili kwa kuwasilisha taarifa zao kwenye mfumo ili kupata TIN kwanza.

Baada ya kuingia kwenye tovuti mshiriki atachagua bidhaa mbalimbali na kuanza kushindana na wengine kwa kuweka bei na atakuwa na uwezo wa kuongeza bei kwa kushindana na wengine.

Pia alisema mshiriki atakayekua ameshinda atataarifiwa kwenye mfumo na anaweza kupata bili kwa ajili ya kufanya malipo ambapo mshindi atapata hati kuruhusu mzigo kutolewa na forodha kwa njia ya mtandao pia.

Mizigo itakayohusishwa na kufanyiwa minada kwa njia ya mtandao ni ile kwa mujibu wa sheria kifungu namba 34 cha sheria ya Forodha Afrika Mashariki ya mwaka 2004 ambapo mizigo inatakiwa iwe imetengenezewa kadhia ya forodha ndani ya siku 21 tangu kuanza kushushwa kutoka kwenye meli, ndege, au malori.

Hata hivyo ikiwa mizigo hiyo haijaondolewa kwenye maeneo hayo ya forodha ndani ya muda huo kifungu cha 42 cha sheria hiyo kimeweka muda wa siku 30 kwa mwenye mzigo awe ametoa mzigo wake na kama siku zimepita sheria inaitaka TRA itangaze kwenye mgazeti na kutoa siku 30 awe amelipia .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles