33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yaelezea umuhimu wa TIN kwenye uchumi

Tanzania-Revenue-Authority

NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

KATIKA kuhakikisha kila mlipa kodi anatambulika, Tanzania ilianzisha utaratibu wa kuwatambua walipakodi wake kwa Namba ya Utambulisho wa mlipa kodi (TIN)

Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kifungu cha 133 inamtaka kila aliye na mapato ajisajili katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndani ya siku 15 tangu kuanza kwa biashara yake.

TIN ni namba itolewayo kitaalamu kwa teknolojia ya kompyuta na hivyo kuwa namba ya kipekee isiyoingiliana na namba nyingine.

Namba hii ya utambulisho hutolewa kwa mlipa kodi na kwamba ndiyo itakayokuwa utambulisho wake katika shughuli zake za kibiashara.

TRA  sasa imeamua kubadili kutoka mfumo wa zamani na kutumia huu wa sasa wa kuhifadhi kumbukumbu za walipa kodi kwa kuweka mfumo mpya unaoendana na ukuaji wa tekinolojia.

Pia kuwa na idadi kamili ya walipa kodi wake wanaostahili kuwepo kwenye wigo wa kodi na kuwaondoa walipa kodi hewa na wale ambao wamekuwa hawajihusishi na biashara kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vifo au kufungwa kwa makampuni au biashara.

Kuwezesha gharama za ulipaji wa kodi kuwa nafuu na kuwawezesha walipa kodi kutimiza majukumu yao ya ulipaji wa kodi kwa hiyari bila shuruti.

Pia kila anayestahili kulipa kodi anatakiwa kupata TIN yakeb  ili aweze kufanya shughuli zake za kiuchumi kihalali bila usumbufu wowote ikiwa ni pamoja na wale wote wanaoanzisha biashara mpya. Hivi basi ndio maana TRA hivi karibuni ilizindua zoezi la uhakiki na uboreshaji wa TIN kwa lengo la kupata taarifa kamili za walipa kodi wake pamoja na kusajili walipa kodi wapya ili kuongeza idadi ya walipa kodi na aina ya kodi.

Kwa mujibu wa Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, George Haule anasema mtu yeyote anaweza kupata TIN na kwamba kuna aina mbili za TIN ambazo ni TIN ya mtu binafsi na ile ya biashara.

Anasema TIN zote zinapatikana TRA hivyo mtu akitaka kupata TIN kwaajili ya biashara atatakiwa kwenda TRA kwaajili ya kujisajili hivyo atapewa fomu ya maombi ambayo baada ya kuijaza ataiambatanisha na barua ya utambulisho wa makazi, picha mbili, mkataba wa pango la sehemu ya biashara (kama amepanga) pamoja na kitambulisho cha kudumu kama kitambulisho cha kupigia kura, kitambulisho cha uraia, hati ya kusafiria au kitambulisho chochote kulingana na mahitaji ya mamlaka.

Sheria hairuhusu mtu mwingine kumchukulia mtu TIN na badala yake muhusika ndiye anayetakiwa kufika TRA kwaajili ya kuchukua na kwamba baada ya kukamilika kwa zoezi la ujazaji wa fomu pamoja na viambatanisho, mtu huyo atatakiwa kuchukuliwa alama za vidole pamoja na kupigwa picha ili taarifa zake zilizo sahihi ziweze kuingizwa katika mfumo pamoja na kuepuka mtu kuwa na TIN zaidi ya moja.

Baada ya taarifa za muombaji wa TIN kuingizwa katika mfumo na kutambulika kama mlipa kodi atapewa hati yenye namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN Certificate) ambayo hutolewa na Kamishna wa TRA.

TIN ni muhimu kwa sababu inamuwezesha mtu kusajili au kubadilisha hati ya kumiliki ardhi, kupata leseni ya udereva, kusajili gari au kuhamisha miliki ya gari, kupata leseni ya biashara na ya viwanda, kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi au kufanya biashara ya uwakala wa forodha wa kutoa mizigo bandarini, kuingia mikataba au kupata zabuni ya utoaji huduma au bidhaa ikiwa ni pamoja na kusajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) hii inamtaka mtu awe na TIN ya biashara.

Pamoja na umuhimu pia TIN ina faida kwa wafanyabiashara kutokana na kuwa itawawezesha kutambulika kuwa ni wafanyabiashara halali.

Wafanyabiashara wenye TIN ndio pekee wanaostahili kumiliki soko la ndani na nje kutokana na kuwa wao pekee ndio watakaoweza kupewa zabuni, leseni, mikopo ya biashara, kandarasi ikiwa ni pamoja na uingizaji nchini na utoaji bidhaa nje ya nchi.

Faida nyingine ni kwamba, wafanyabiashara wenye TIN wanalindwa na sheria dhidi ya ushindani usiokuwa wa halali.

Mbali ya wafanyabiashara, pia serikali itafaidika kutokana na kuwa  na wigo wa kodi unaoongezeka na kuiwezesha kuongeza pato lake ambalo litaiwezesha kutoa na kuboresha huduma za jamii na uchumi.

Ukwepaji wa kodi utathibitishwa, itachochea kukua kwa uchumi kwa kutoa mazingira bora ya ushindani wa haki kibiashara kwa kudhibiti biashara za mifukoni ikiwa ni pamoja na kurahisisha upashanaji wa taarifa kati ya idara au taasisi mbalimbali za serikali na hivyo kuboresha huduma na kudhibiti ukwepaji wa kodi.

Kwa mujibu wa TRA, TIN hutolewa bila malipo yoyote na kwamba watu wasiostahili kujisajili ili kupata namba hii ya utambulisho ni wale wasio na mapato yatozwayo kodi au waajiriwa ambao mapato yao yote hutozwa kodi kwa mpango wa PAYE.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles