25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

TRA sasa kupita nyumba kwa nyumba

Richard Kayombo

NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), inatarajia kugawa maeneo kama vitalu ili kuweza kuwafikia wafanyabiashara wote waweze kulipa kodi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa semina ya siku mbili iliyofanyika katika Ukumbi wa APC uliopo katika ofisi za makao makuu ya NBAA, Bunju na kuwahusisha wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema kila mtumishi wa mamlaka atapewa eneo lake ambalo atatakiwa kujua kila biashara inayofanyika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila mfanyabiashara analipa kodi.

Alisema pia mtumishi huyo atatakiwa kuhakikisha anasikiliza matatizo ya kila mfanyabiashara na kuyatatua na kwamba katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa wameajiri watumishi zaidi ya 300 na wanatarajia kuongeza wengine 100.

Alisema watakuwa wakizunguka mitaa yote ikiwa ni pamoja na nyumba hadi nyumba kutokana na kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakifungua viwanda kwenye nyumba wanazoishi.

“Tutahakikisha tunajiimarisha kwa kuongeza watumishi wa kutosha ili tuweze kufanikisha zoezi la ukusanyaji wa kodi kutoka kwa kila mfanyabiashara,” alisema Kayombo.

Naye Mwenyekiti wa mkutano huo, Juma Muhimbi, alisema lengo la mkutano huo uliowakutanisha TRA na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), ni kujadili mapendekezo ambayo yatakuwa mchango katika bajeti ya Serikali ya mwaka mpya wa 2017/18 ambapo leo ndio wanatarajia kuyajadili.

Alisema katika mkutano huo, jana walijadili mapendekezo waliyoyatoa mwaka jana kwa ajili ya mwaka huu ambayo mafanikio yake yameweza kuleta mabadiliko katika bajeti ya mwaka huu iliyopitishwa na Serikali ya awamu ya tano.

Alisema walitoa mapendekezo katika masuala mazima ya kodi ambapo Serikali kwa kutumia mapendekezo hayo imeipa kibali TRA cha kukusanya kodi ya majengo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wateja wasioomba risiti baada ya kumaliza manunuzi ya bidhaa mbalimbali pamoja na kuwanyang’anya leseni kwa muda wa miaka miwili wafanyabiashara wote ambao watabainika kutotoa risiti kwa makusudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles