KOKU DAVID-DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema mfanyabiashara ana haki ya kupata taarifa zinazohusiana na kodi, mabadiliko ya sheria za kodi, tozo na ada mbalimbali anazotakiwa kulipa.
Akizungumza jijini Dar es Salam, Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Diana Masala, amesema kuwa pamoja na kujua haki zake anatakiwa kupata elimu ya mara kwa mara itakayomuwezesha kuwa na utayari wa kulipa kodi kwa hiyari.
Amesema katika kuelekea uchumi wa kati wa viwanda serikali imepunguza baadhi ya kodi ili kuvutia wawekezaji na kwamba punguzo hilo litahusu wawekezaji wote wa ndani na nje.
Amesema kwa upande wa wafanyabiashara binafsi, kodi ya mapato hutozwa kutokana na mauzo yao na kwamba katika mwaka wa fedha wa 2019/20 viwango vya kodi vimepunguzwa na kwa mfanyabiashara binafsi atakayekuwa ametunza kumbukumbu zake atanufaika zaidi na punguzo hilo.