23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

TRA : Kila mfanyabiashara Kariakoo lazima awe na mashine ya EFD

prima

NA KOKU DAVID,

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kufanya vizuri katika suala zima  la kukusanya mapato ya serikali na kuvuka lengo.

Katika kuhakikisha inafanikiwa kukusanya na kuvuka lengo la mwaka wa fedha wa 2016/17 la kukusanya sh trilioni 15.1, TRA imekuwa ikitoa elimu ya kodi kwa jamii ikiwa ni pamoja kupanua wigo wa walipa kodi.

TRA imeweka mikakati mbali mbali ambapo miongoni mwa mikakati hiyo ni kutoa elimu ya kodi, kuboresha huduma zake, kusajili walipa kodi wapya ili kuongeza wigo wa kukusanya kodi ikiwa ni pamoja na kuipa hadhi Kariakoo kuwa Mkoa Maalumu wa Kodi.

Yote haya iwapo yatafanikiwa, basi TRA itakusanya mapato mengi ambayo yatawezesha nchi kufanya mambo mbalimbali ya maendelea katika jamii.

Tangu kuingia kwa serikali ya awamu ya tano, TRA imekuwa na mikakati thabiti ya kuweza kufanikisha suala la ukusanyaji mapato hali iliyoifanya mamlaka hiyo tangu Desemba mwaka jana imekuwa ikifanya vizuri katika idara ya ukusanyaji wa kodi.

Katika kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato pamoja na kukusanya mapato kikamilifu, hivi karibuni TRA imelifanya eneo la Kariakoo kuwa mkoa maalumu wa kodi kutokana na kuwa kitovu cha biashara nchini.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo anasema pamoja Kariakoo kuwa Mkoa wa Kodi pia watahakikisha kila mfanyabiashara anakuwa na mashine za kodi za kielektroniki (EFD) na kuitumia ipasavyo kwa mujibu wa sheria.

Anasema katika kutekeleza hilo, mawakala wa EFD wamefungua ofisi ya pamoja maeneo ya Kariakoo mtaa wa Msimbazi ili kuwarahisishia namna ya upatikanaji wa mashine hizo ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto watakazokutana nazo wakati wa kuzitumia.

Kila mfanyabiashara anatakiwa kuwa na mashine ya EFD ambayo kazi yake kubwa ni kutunza kumbukumbu za biashara ikiwa ni pamoja na kuiwezesha TRA kutambua mauzo yaliyofanyika na kodi inayotakiwa kulipiwa.

Pia wanunuzi wa bidhaa wanatakiwa kuhakikisha kila wanapokamilisha manunuzi wanadai risiti zitokanazo na mashine ya EFD ili kodi wanazolipa kutokana na manunuzi wanayofanya iweze kufika moja kwa moja serikalini.

Sambamba na hilo pia kila mtu anayestahili kuwa na Namba ya Utambulisho (TIN) anatakiwa kufika katika vituo mbalimbali ambavyo vinatoa huduma hiyo ili waweze kuhakiki taarifa zao ikiwa ni pamoja na kuiwezesha TRA kujua idadi ya walipa kodi wao.

Kwa mujibu wa TRA zoezi la uhakiki wa TIN kwa mkoa wa Dar es Salaam ambako limeanzia hautaongezwa na badala yake litahamia katika mikoa mingine.

Zoezi hili ni miongoni mwa mikakati iliyowekwa na TRA kufanikisha ukusanyaji wa mapato na kwamba wananchi wanatakiwa kujitokeza ili kuweza kuisaidia mamlaka hiyo kufikia malengo yake kulingana na mikakati iliyojiwekea.

Ili mfanyabiashara aweze kufanya biashara yake kwa uhuru, TRA inawashauri kufika katika ofisi zake ili kujisajiri kuepuka usumbufu wa kutozwa faini zisizo za lazima.

Mbali na TIN, pia kila mfanyabiashara wakiwemo wamiliki wa vituo vya mafuta wanashauriwa kununua mashine za EFD kabla ya Septemba 30 kutokana na kuwa TRA inatarajia kuanza msako wa wafanyabiashara wasiokuwa na mashine hizo Oktoba mosi na wale watakaokiuka hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.

Kwa upande wa wafanyabiashara waliosajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) wanashauriwa kuwasilisha taarifa za biashara zao kila terehe 20 ya mwezi badala ya 27 iliyokuwepo awali kabla ya mwaka huu wa fedha.

Na kwa wale walipa kodi za makadirio na kodi za makampuni wanatakiwa kulipa  zao mapema mwezi Septemba ili kuepuka usumbufu wa msongamano wa mwisho wa mwezi.

Hadi sasa tangu kuanza kwa mikakati hiyo, TRA imeweza kuona matunda yake kwa haraka kutokana na makusanyo ambayo wameweza kukusanya ambapo kwa mwezi Agosti wameweza kukusanya sh trilioni 1.158 ikilinganishwa na lengo la kukusanya sh trilioni 1.152 ambayo ni sawa na silimia 100.57.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles