TRA: Atakayefichua wakwepa kodi atalipwa 3%

0
695

VERONICA KAZIMOTO-SIMIYU

MENEJA wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Diana Masalla, amesema mwananchi yeyote atakayefichua wakwepa kodi na TRA ikafuatilia na hatimaye kodi hiyo ikagundulika ni kweli ilikuwa imekwepwa na ikakusanywa, atalipwa asilimia 3 ya kodi iliyokusanywa lakini haitazidi Sh milioni 20.

Diana aliyasema hayo wakati wa Jukwaa la Biashara na Uchumi lililofanyika wilayani Busega mkoani Simiyu, ambalo lengo lake ni kujadili fursa, changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wilayani humo na kuzitafutia ufumbuzi.

“Natoa wito kwa wananchi na washiriki wa jukwaa hili kuhakikisha mnawafichua wakwepa kodi wote kwa sababu watu hao wanaiibia Serikali yetu mapato na wanarudisha nyuma jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wake,” alisema Diana.

Pamoja na hayo, aliwahimiza wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki jukwaa hilo kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa pindi wanapokuwa wamefunga biashara kutokana na sababu mbalimbali ili kuepuka kuendelea kutozwa kodi au kuonekana wamekaidi kulipa kodi.

“Ni muhimu kutoa taarifa TRA pale ambapo mfanyabiashara amefunga biashara yake, lakini pale anapofungua ni muhimu pia kuitaarifu TRA ili kuepuka kuendelea kutozwa kodi unapofunga biashara, na pia kuanza kutozwa kodi sahihi pale unapofungua biashara,” alisema Diana.

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Busega, David Mateko, alimpongeza Meneja wa TRA Mkoa wa Simiyu kwa kutoa elimu ya kodi kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara mkoani humo pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na hatimaye kuifanya Wilaya ya Busega kuwa ya pili kati ya wilaya tano za Simiyu kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yanayosimamiwa na TRA.

“Nampongeza Meneja wa TRA katika mkoa wetu wa Simiyu kwa kuwatembelea wafanyabiashara na kuwapatia elimu ya kodi na pia nachukua fursa hii kumpongeza Mkuu wetu wa Wilaya, Tano Mwera kwa kutuhamasisha kulipa kodi kwa wakati na sasa wilaya yetu imekuwa ya pili hapa mkoani kwa ukusanyaji mapato yanayosimamiwa na TRA,” alisema Mateko.

Jukwaa hili la biashara na uchumi wilayani Busega limewakutanisha wafanyabiashara na wawekazaji zaidi ya 200 ambapo taasisi mbalimbali za Serikali zimealikwa kutoa mada ikiwa ni pamoja na TRA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here