29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

TPSF KUTAFUTA WAWEKEZAJI MKAKATI KUTOKA JAMHURI YA CZECH

Na LEONARD MANG’OHA


SERIKALI ya Awamu ya Tano chini wa Rais Dk. John Magufuli, imeendelea na juhudi zake za kuhakikisha inakuza uchumi unaotegemea sekta ya viwanda ambavyo vitazalisha ajira nyingi.

Katika juhudi hizo, tayari viwanda kadhaa vimeshajengwa katika maeneo mbalimbli vikiwamo vya vinywaji baridi vitokanavyo na matunda, vigae, sabuni na bidhaa nyingine za urembo.

Hadi Desemba mwaka jana, zaidi ya Kampuni 130 zilikuwa zimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwekeza hapa nchini, huku baadhi ya kampuni hizo zikianza ujenzi tangu Januari mwaka huu kwa matarajio kuanza uzalishaji ifikapo Julai mwaka huu.

Huu ni mwelekeo chanya katika kuelekea dira ya uchumi wa viwanda unaolengwa na Serikali katika kupunguza umasikini kwa kuongeza fursa za ajira zitakazosaidia kuboresha kiwango cha maisha.

Kuongezeka kwa kasi kwa wawekezaji hususani wale wa nje ya nchi, kumechagizwa zaidi na uhusiano baina ya Tanzania na mataifa ya kigeni, ambapo tumeshuhudia mikataba kadhaa ikisainiwa kati yetu na mataifa kama vile Uturuki, China, Morocco, Ethiopia na mataifa mengine duniani sanjari na mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Wiki iliyopita TIC katika taarifa yake iliyochapishwa katika gazeti hili, ilieleza kufanyika kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Jamhuri ya Czech litakalofanyika Mei 2, mwaka huu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kongamano hilo litawakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Czech kujadiliana fursa kadha wa kadha za kibiashara zitakazowezesha kuanzisha na kuendeleza miradi ya viwanda, kupata wabia watakaokuwa tayari kutoa mitaji kwa wafanyabiashara wazawa kukuza teknolojia na kupata masoko.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sekta zilizolengwa ni pamoja na sekta ya kilimo ambapo watajikita katika mazao ya korosho, viungo, kahawa, chai, mahindi, pamba, katani alizeti na ufuta.

Pia utahusisha teknolojia ya mawasiliano, utalii, madini na biashara kwa ujumla wake.

"Tunategemea Tanzania itaongeza thamani ya mitaji ya uwekezaji kutoka nje (FDI) iwapo makampuni ya wafanyabiashara kutoka Czech yatakubaliana kufanya biashara na kuwekeza Tanzania," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kumekuwapo na mialiko mbalimbali ya makongamano ndani na nje ya nchi inayohusisha wafanyabiashara wa ndani na wa kigeni kwa lengo la kuonesha fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana katika nchi shiriki.

Jambo la msingi ni kufahamu kama makongamano hayo hutumika vizuri kusaidia kukuza uchumi wetu au tunatumia makongamano hayo kuwaonesha wageni kuwa sisi ni soko la kupokea bidhaa wanazozalisha kwao.

Ili kupatikana tija ya makongamano na ushirikiano kati yetu na mataifa ya kigeni, ni lazima kuwapo kwa mipango mkakati wenye faida kwa pande zote mbili (yaani win win situation).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye, anasema yanapoandaliwa makongamano ya aina hiyo, Serikali yetu inapaswa kuwa na agenda yake maalumu ambayo wataisimamia na kuieleza kwa washiriki kwa lengo la kupata wawekezaji.

Anasema kwa mfano katika kongamano la Czech, Tanzania inapaswa kwenda na agenda ya kutafuta kampuni chache zitakazokuwa tayari kuja nchini kuwekeza katika sekta ya kilimo hususani cha alizeti na ufuta mazao anayoamini yanaweza kuivusha Tanzania kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji.

Anashauri kuwa kampuni hizo zinaweza kukaribishwa kuonana na rais na kuzungumza naye na wakakubaliana ziwekeze katika kilimo cha mazao hayo pamoja na kujenga viwanda vya kuzalisha mafuta yatakayouzwa nje ya nchi badala ya kuuza malighafi.

Anaongeza kuwa uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini  ni mdogo kuliko mahitaji kutokana na wakulima wengi kuendelea kupata mavuno ya gunia tano kwa ekari moja huku wachache wakifikia gunia 25.

"Nitakwenda katika mkutano huo, kwa sababu nitakuwa na nafasi ya kuchangia nitachagiza  uwekezaji wenye maana utakaowezesha kuinua sekta binafsi, si kuwaonesha kuwa tuna fursa fulani bila kuwashawishi kwa dhati kuwekeza katika maeneo muhimu.

“Czech wana teknolojia nzuri na wazalishaji wazuri wa mazao mbalimbali, kwani hata mataifa ya Ulaya kama Ujerumani yananunua bidhaa nyingi kutoka huko," alisema Simbeye

Kwa sababu nia ya Serikali ni kuhakikisha inaongeza uzalishaji katika sekta ya viwanda ili vilete tija na kupunguza tatizo la ajira, haina budi kuzielekeza idara zake kutumia wataalamu wa uchumi waliopo kutafuta njia bora zaidi ya kuongeza ufanisi wa sekta hiyo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles