33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

TPB: TUNAAMINI KUWAFIKISHIA WATEJA HUDUMA BORA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


SEKTA ya benki ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo ndio maana kumekuwa na ongezeko kubwa la taasisi za kifedha nchini.

Licha ya umuhimu wa sekta hiyo, utumiaji wa huduma za kibenki nchini bado uko chini kwani ni asilimia 17 tu ya Watanzania ndio wenye akaunti katika mabenki.

Kulingana na ripoti ya kitaifa kuhusu upatikanaji na utumiaji wa huduma za kifedha nchini (Finscope) iliyotolewa hivi karibuni, hali hiyo inachangiwa na huduma kuwa mbali na wananchi.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa Watanzania wengi wanaamini kwamba fedha zao huwa salama zaidi zikiwa ndani ya benki kuliko sehemu nyingine yoyote.

Ili kupanua wigo wa huduma za kifedha kwa wananchi na kuweza kufanikisha ukuaji wa uchumi kwa maendeleo ya Taifa, utafiti huo ulipendekeza watoa huduma kuziboresha kwa mnaana ya kuzisogeza karibu na kubuni bidhaa mbalimbali zitakazokidhi mahitaji ya wananchi.

Mwaka huu katika kuboresha mazingira ya kazi kusogeza huduma karibu na wananchi, Benki ya TPB iliamua kufungua tawi jipya katika Wilaya ya Temeke.

Kabla ya kufunguliwa kwa tawi hilo jipya, awali kulikuwa na tawi dogo lililokuwa katika ofisi za Shirika la Posta zilizoko Temekemwisho ambalo lilikuwa na nafasi finyu na kusababisha wateja kulalamika kwa ufinyu wake.

“Tuliamua kukodisha jengo hili (mahali lilipo tawi jipya) na kuanza kufanya ukarabati, na tangu Julai lilikuwa liko tayari kuweza kuwahudumia Watanzania.

“Wateja wetu walikuwa wakilalamikia nafasi finyu iliyokuwepo pale Temeke Mwisho, lakini naamini sasa watayafurahia mazingira haya mazuri yenye nafasi ya kutosha,” anasema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB, Sabasaba Moshingi.

Anasema wanaendelea na utafiti wa kuweza kujua ni namna gani wataweza kuwafikia watu wengi zaidi katika huduma za kibenki zenye lengo la kukuza uchumi wa nchi.

“Bado huduma za kibenki hazijawafikia Watanzania wengi, huduma ziko mbali na wananchi lakini sisi tunaamini katika kuwafikishia wateja wetu huduma na kutoa uelewa mpana kuhusu hali ya huduma za kifedha nchini,” anasema.

Ofisa Mtendaji huyo anasema wanaendelea kuboresha huduma ili kuwanufaisha watu wengi hasa wa kipato cha chini.

Anazitaja baadhi ya huduma zitakazotolewa katika tawi hilo kuwa ni huduma ya kuweka akiba, akaunti maalumu ambayo riba yake ni asilimia 10, huduma za mikopo ya vikundi kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, wa kati na wakubwa.

“Tumejitahidi sana kuboresha benki yetu, huduma tunazo nyingi na za kisasa, tunatoa mikopo ya vikundi mfano kwa mama ntilie, wamachinga, bodaboda na wengine waungane waje tutawapa mikopo.

“Kuna mteja wetu mmoja Arusha alianza kukopa Sh 500,000 lakini kutokana na kuwa na nidhamu katika urejeshaji mikopo hivi sasa anaweza kukopa hadi Sh milioni 300 na analipa kwa mwaka mmoja,” anasema Moshingi.

Naye Meneja wa TPB tawi la Temeke, Epaphro Mwego, anasema huduma za kifedha ni muhimu kwa watu kujiendeleza na kujikwamua kiuchumi hivyo anaamini tawi hilo litaongeza idadi ya wateja kwenye benki yao.

“Tunatarajia kuwa tawi hili litaongeza idadi ya wateja watakaofika kupata huduma mbalimbali tunazozitoa hivyo nawakaribisha wananchi wote wa Temeke na wengine kufika kwenye tawi hili, tutawapatia huduma bora za kibenki,” anasema Mwego.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles