32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

TPA yatakiwa kuendelea kuboresha bandari ziwa Viktoria

Na Clara Matimo, Mwanza

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) kuhakikisha inaendelea kuboresha bandari katika Ziwa Viktoria ili meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu iweze kutia nanga bila shida itakapoanza kufanya  safari zake katika nchi zote ambazo ziko ukanda wa ziwa viktoria.

Agizo hilo limetolewa jijini Mwanza leo Februari 12, 2023 na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Pro. Makame Mbarawa kwenye hafla ya kushushwa  majini meli hiyo katika bandari ya Mwanza Kusini iliyopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza ambayo inajengwa  kwa gharama ya  zaidi ya Sh bilioni 109.  

Baadhi ya wananchi na viongozi wakishuhudia tukio la kihistoria la kushushwa majini meli  ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ambayo ni kubwa  kuliko zote zinazoelea katika maziwa makuu nchini yenye uzito wa tani 3000 ikiingizwa majini ziwa viktoria katika bandari ya Mwanza Kusini  iliyopo Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza,

Amesema Serikali imekuwa ikiwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ya  usafiri nchini lengo ni kuboresha huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria kwa wananchi wake hivyo itakapoanza kufanya safari zake kusiwepo na changamoto ya bandari kwenye maeneo itakayopita hasa ikizinngatiwa kuwa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ni meli kubwa zaidi kuliko zote zinazoelea katika maziwa makuu nchini.

Vile vile Mwakibete ameielekeza Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL) kusimamia menejimenti ya MSCL miradi yote inayotekelezwa na itakayotekelezwa na Serikali ikamilike kwa wakati ikiwa na thamani halisi ya fedha zilizotumika katika kuijenga iweze kuwanufaisha  wananchi  kwa muda mrefu ili kutimiza lengo la  Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliyedhamiria kuwapa huduma bora wananchi wake.

Akitoa taarifa fupi ya kihandisi Meneja Mradi wa Ujezi wa Meli hiyo, Mhandisi Vitus Mapunda amesema meli hiyo inatarajiwa kutoa huduma kwa kipindi kisichopungua miaka 50 kwa kuwa  itafanya safari zake ndani ya ziwa viktoria ambalo maji yake hayana chumvi hivyo hayatafanya uharibifu wa vifaa.

“Nawahakikishia watu wote watakaotumia meli hii itakapokamilika kwamba imejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa hivyo itakuwa na usalama wa kutosha kabisa na haitakuwa na uchafuzi wa mazingira kutokana na usanifu uliofanyika, tumeifanyia majaribio mengi ya kisayansi ya kompyuta,”amesema Mhandisi Mapunda.

Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL, Mhandisi Eric Hamissi(mwenye suti wa kwanza kulia) akiwa ameketi meza kuu  katika hafla ya kuishusha majini Meli Mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu anayefuata(aliyevaa suti pia) ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete.

Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL, Mhandisi Eric Hamissi amesema ujenzi wa meli hiyo unaofanywa na Mkandarasi kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini ulianza Januari 2019 hadi sasa umekamilika kwa asilimia 82 ukikamilika utarahisisha shughuli  za usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo maana ni meli ambayo  itakuwa na mwendo kasi zaidi kuliko meli zote zinazoelea katika ukanda wa maziwa makuu.

“Tangu kuundwa kwa misingi ya dunia ziwa hili viktoria halijawahi kubeba uzito kama ambao limeubeba leo kwa kuwa meli hii ni kubwa sana itakapokamilika itakuwa na uzito wa tani 3500 leo tumeingiza ndani ya maji tani 3000  tukio hili ni la kihistoria, MV Mwanza Hapa Kazi Tu ina urefu wa mita 92.6, kimo ghorofa nne, upana mita 17 hata nyie mnaiona ilivyokubwa, “amesema Mhandisi Hamissi na kuongeza.

Amefafanua kwamba meli hiyo ikikamilika itakuwa na madaraja sita ambayo ni daraja la hadhi ya juu kabisa(VVIP), watu mashuhuri(VIP) la kwanza(first class) la pili (second class) biashara(business) na uchumi(economic).

“Kutakuwa na lifti ambayo inauwezo wa kubeba watu 20 kwa wakati mmoja kwa ajili ya abiria ambao wanachangamoto ya kupanda ngazi na wagonjwa, migahawa ya kisasa, sehemu ya kucheza muziki, dispensary, ukumbi wa kufanyia sherehe wenye uwezo wa kubeba watu 400,” ameeleza  Mhandisi Hamissi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika hafla hiyo wakuu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa akiwemo Adam Malima wa Mwanza na Albert Chalamila wa Kagera  wamesema mradi huo ukikamilika utachangiza maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla kwani usafiri wa meli ni wa gharama nafuu zaidi.
 pia utawezesha kusafirisha shehena kubwa ya mizigo kwa wakati mmoja.

“Wakazi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa tunayo kila sababu ya kumshukuru Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan  kwa uamuzi wake wa kuendelea kuwekeza fedha nyingi sana katika mradi huu  pamoja na miradi mingine ya maendeleo ya kimkakati iliyopo mikoa ya kanda ya ziwa mradi huu ukikamilika utawasaidia wananchi ambao ni wafanyabiashara kusafirisha shehena kubwa ya mizigo kwa wakati mmoja,”ameeleza Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi  Kakoso, amewasihi watumishi wa MSCL kuitunza meli hiyo ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu itakapokamilika ili idumu kwa muda mrefu iweze kuwanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.  

“Huko nyuma tulikuwa na meli nyingi ambazo zilikuwa za serikali lakini zilipotea kutokana na baadhi ya watumishi kukosa uzalendo, tunategemea MSCL mtaitunza meli hii na mtaifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu za kisheria,”amesisitiza Kasoko.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,400FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles