Na JUDITH NYANGE
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imezilipa fidia Sh bilioni 5.6 kaya 144 zilizopisha eneo la ukubwa wa ekari 1,178 kwa ajili ya bandari kavu ya mizigo inayotarajia kujengwa katika vitongoji vya Nyakilingi na Budo katika Kijiji na Kata ya Fela wilayani Misungwi.
Meneja wa Bandari ya Mwanza, Daniel Sira, alikuwa akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela aliyetembelea eneo hilo na kuwakabidhi hati baadhi ya wananchi juzi.
Alisema kaya 111 zinatoka katika Kitongoji cha Nyakilingi na 33 Budo.
Alisema baada ya kuzungumza na halmashauri, viongozi wa kijiji na wananchi wote wa maeneo hayo kuhusu mradi huo walionekana kuupokea kwa shangwe kutokana na faida zitakazopatikana wakati wa ujenzi na hata baada ya kukamilika bandari hiyo.
“Katika eneo hilo lililochukuliwa tulikuta nyumba 372 zilizojengwa kwa matofali ya tope na kuezekwa nyasi, 22 za matofali ya saruji na mchanga na kuezekwa kwa bati.
“Nyumba nane za matofali ya kuchoma na zimeezekwa kwa bati, tulikuta misingi sita ya nyumba iliyojengwa kwa mawe, mazao, miti ya asili na ile ya kupandwa.
“Watu 668 wanaotokana na kaya 144 watapata malipo kutokana na mtu moja kumiliki zaidi ya eneo moja, tayari wananchi 651 wameshakabidhiwa hundi zao za malipo ya fidia na wamebaki 17 tu.
“Hao hawakujitokeza lakini malipo yao yapo na tumetoa maelekezo kwa mwenyekiti wa kijiji watakapojitokeza wafike katika ofisi zetu kulipwa,” alisema Sira.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alisema atamshauri waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, kuliwekea uzio eneo hilo litambulike na mipaka yake kuepusha wananchi kulivamia na kuanzisha upya mgogoro wa kudai upya fidia.
“Kuna nguzo nyingi za mipaka kwenye viwanja zimeanza kuibuka kama mchwa, nimepita hapa mwezi mmoja uliopita nilikuwa sioni nguzo nyingi kama nilizoziona leo.
“Maana yake ni watu wameshaona bandari inakuja kila mtu anataka kuhamia huku ni lazima uwepo utaratibu mzuri,” alisema Mongela.
Mongela alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo na mkurugenzi kuweka mpangilio wa makazi katika maeneo ya jirani na bandari hiyo kwa kutenga maeneo ya barabara, shule, vituo vya afya na huduma nyingine za jaamii.