20.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Tope latibua utamu Yanga Vs Mbeya City

WINFRIDA MTOI

MVUA iliyonyesha jana jijini Mbeya, iliathiri kwa kiasi kikubwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kati ya Yanga na Mbeya City, baada ya Uwanja wa Sokoine uliotumika kutuama maji pamoja na tope.

Katika mchezo huo, Yanga na wenyeji wao Mbeya City ziligawana pointi moja moja, baada ya dakika 90 kukamilika kwa suluhu.

Kutokana na hali hiyo, timu zote mbili zililazimika kucheza mchezo wa kubutua usiokuwa wa kiufundi, ili kuendana na mazingira ya uwanja huo.

Hali hiyo iliwafanya wachezaji wa timu zote mbili kushindwa kucheza kwa uhuru na mpira ulikuwa haudundi inavyotakiwa, hivyo muda mwingi walitumia kubutua.

Timu zote zilianza mchezo kwa kushambuliana kwa zamu huku zikicheza kwa kupiga pasi ndefu kutokana na changamoto ya uwanja iliyotokana na mvua iliyonyesha muda mwingi wa kipindi cha kwanza.
Licha ya Yanga kujitahidi kutengeneza nafasi kadhaa kupitia, Patrick Sibomana, David Molinga na Deus Kaseke, mabeki wa Mbeya City walikuwa imara kuhakikisha lango lao linakuwa salama.

Mbeya City ilikuwa ikifanya mashabulizi yake kupitia Peter Mapunda, Selemani Ibrahim na Idd Gamba ambaye dakika ya 30, alipata nafasi nzuri lakini kipa wa Yanga Farouk Shilalo aliweza kuokoa hatari hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, timu kila mmoja akitafuta bao lakini jitihada zao hazikuzaa matunda.

Dakika ya 60, Kocha Mkuu wa Yanga, alifanya mabadiliko, akimtoa Said Makapu na kuingia Mrisho Ngassa.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkwasa alisema walicheza vizuri, lakini kilichowaangusha ni mazingira mabaya ya eneo la kuchezea la uwanja.

Pia aliwatupia lawama waamuzi kwa kushindwa kutafsiri vizuri sheria za mchezo wa soka.

“Uwanja hakuwa mzuri ila mwamuzi aliyecheza mechi yetu ni kati ya wale wanalirudisha nyuma soka la Tanzania, waamuzi kama hawa ni ‘kichefu chefu’,” alisema Mkwasa.

Katika hatua nyingine straika mpya wa kikosi hicho, Ditram Nchimbi, amekwenda kujiunga na timu hiyo Mbeya inayotarajia kushuka tena dimbani keshokutwa kuumana na Tanzania Prisons kwenye uwanja huo huo.

Baada ya suluhu ya jana, Yanga imefikisha pointi 18 na kukamata nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, inayoshirikisha timu 20, ikicheza michezo tisa, ikishinda mitano, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja.

Kikosi cha Yanga: Farouk Shihalo, Mustafa Seleman, Jafary Mohammed, Lamine Moro, Ally Mtoni Sonso, Said Makapu, Deus Kaseke, Papy Tshishimbi, David Molinga Falcao, Raphael Daudi na Patrick Sibomana.

Kikosi cha Mbeya City ni Haroun Mandanda, Keny Kunambi, Hassan Mwasapili, Samson Madeleke, Baraka Johnson, Edgar, Mbembela, Seleman Mangoma, George Chota, Idd Gamba, Peter na Seleman Gamba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,595FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles