Serikali imesema si rahisi kuagiza tohara kwa wanaume nchini kuwa lazima ingawa ina faida kiafya kulinganisha na athari zake.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khamisi Kigwangala amesema hayo bungeni leo Septemba 12 wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) ambaye aliitaka serikali kuagiza tohara kwa wanaume liwe ni jambo la lazima kwani imethibitika kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa kiasi kikubwa.
Dk. Kigwangala amesema, wizara iliweka mikakati ya kubaini mikoa ya kipaumbele ambayo haina utamaduni wa kutahiri na ina kiwango cha maambukizi ya VVU na kutoa huduma ya tohara ambapo pia amewataka wanawake kuwashauri wanaume kufanya tohara.
“Serikali iliendesha kampeni kubwa ya tohara maarufu ‘Dondosha mkono wa sweta’ ambapo elimu kuhusu tohara ilitolewa kupitia matangazo na vipindi vya redio na televisheni, mabango, machapisho,vijarida mbalimbali, filamu na wa elimisha rika,”amesema.
Aidha, Dk. Kigwangalla ameitaja mikoa ambayo haina utamaduni wa kufanyiwa tohara kuwa ni Iringa, Njombe, Tabora, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera na Mara.