27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

TMA yatahadharisha kutokea kwa vimbunga pacha Bahari ya Hindi

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetahadharisha kuwapo kwa uwezekano wa kutokea kwa vimbunga pacha magharibi mwa Bahari ya Hindi upande wa kaskazini na kusini mwa Ikweta na hivyo kuwa na uwezekano wa kuathiri mifumo ya hali ya hewa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya mamlaka hiyo, migandamizo hiyo midogo pacha inaelekea kuimarika na kuwa vimbunga katika Pwani ya Somalia (Upande wa Kaskazini mwa Ikweta ) na Kaskazini Mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar (Kusini mwa Ikweta).

“Aidha, mgandamizo mdogo wa hewa uliopo kusini magharibi mwa bahari ya Hindi (karibu na kisiwa cha Madagascar) unatarajiwa kuimarika na kuelekea kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar, na hivyo unatarajiwa kusababisha ongezeko la mvua pamoja na vipindi vya mvua kubwa hususan katika baadhi ya maeneo ya Pwani ya Kaskazini ya nchi yetu kati ya Desemba 5 na 6, mwaka huu.

“Mamlaka inaendelea kutoa tahadhari ya vipindi vifupi vya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma,” imesema taarifa hiyo.

Pamoja na mambo mengine taarifa hiyo imetanabaisha kuwa kwa upande mwingine, mgandamizo mdogo wa hewa katika pwani ya Somalia unatarajiwa kuendelea kuwa mbali na pwani ya Tanzania na hautarajiwi kuwa na madhara katika nchi yetu.

“Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zitakazotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalamu katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza,” imesema.

TMA imesema inaendelea kufuatilia hali hiyo katika bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa kwa ujumla na itatoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles