29.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

TIZEBA HATANIWI KIKAZI

  • Aonya vyama ushirika ucheleweshaji malipo 
  • Apiga marufuku biashara ya ‘Butura’ shambani

Na Mwandishi Wetu


WAZIRI wa Kilimo Dk. Charles Tizeba ameanza kukunjua makucha dhidi ya watendaji wanaokwamisha mambo ndani ya wizara yake.

Dk. Tibeza amekuwa mkali dhidi ya watendaji wake, baada ya kufanya ziara ya siku tatu mkoani Kagera na kubaini udhaifu katika maeneo mbalimbali ambayo anaamini kama yakisimamiwa vizuri, ni wazi kero zilizopo zikiondolewa mambo yatakwenda vizuri.

Julai 10 hadi 13, mwaka huu, kwa nyakati tofauti   alitembelea wilaya za Bukoba, Kyerwa, Karagwe, Missenyi na Muleba ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu, Dar es Salaam.

Katika maagizo hayo, Rais Dk. Magufuli aliitaka Wizara ya Kilimo kufuatilia sababu za wakulima wa zao la Kahawa kucheleweshewa malipo, huku wengi wao wakiuza kahawa nchini Uganda.

Kabla ya kwenda Kagera, Waziri Dk. Tizeba, ali alimwagiza naibu wake, Omary Mgumba ambaye alibaini changamoto za uuzaji wa kahawa na kero nyingi kwa wananchi.

Moja ya changamoto kubwa aliyokutana nayo, ni vyama vya ushirika vikuu vya KCU na KDCU kuchelewesha malipo ya wakulima.

Akiwa mkoani humo, Waziri Tizeba alikutana na makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupokea taarifa ya mkoa huo iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu kuhusu sekta ya kilimo hususani zao la kahawa, kukutana na wadau wa kahawa, kutembelea vyama vya msingi na kukutana na wadau wa kahawa na viongozi wa viwanda.

Marufuku

Akizungumza na wadau wa zao la kahawa wilayani Kyerwa, Dk. Tizeba alikemea vikali biashara ya kuuza kahawa nje ya nchi pasipo kufuata utaratibu wa kisheria.

“Acheni kuuza kahawa mbichi nje ya nchi, haya ni magendo, atakayebainika kuendelea na biashara hii atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.”

Pia alizuia wananchi kuuza kahawa mbichi, ikiwa bado iko shambani na haijakomaa (Butura), kwani kufanya hivyo ni kudhoofisha na kuzorotesha juhudi za muda mrefu alizotumia mkulima  na kumkosesha mapato stahiki.

Alisema Serikali itajitahidi kutafuta bei nzuri ya zao la kahawa ndani na nje ya Afrika Mashariki ili wananchi wapate faida na tija ya kilimo.

Kutokana na hali hiyo, alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa,Shadrack Mhagama kukamilisha haraka iwezekanavyo kiwanda cha kukoboa kahawa cha Omkagando kilichozinduliwa  wakati wa mbio za  Mwenge wa Uhuru  mwaka 2016 kwa gharama za Serikali lakini mpaka sasa kimeshindwa kuendelezwa.

Ubadhirifu

Alitangaza kupambana na viongozi wa vyama vya msingi ushirika kutokana na kuwapo tuhuma za ubadhilifu.

“Viongozi na baadhi ya watendaji wa vyama vya ushirika wanaofanya ubadhirifu wa mali za ushirika kwa manufaa yao, nasema nitapambana nao kwa kila hatua.

“Ubadhirifu huu unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika, umekuwa ni tatizo sugu na hata kuwakatisha tamaa wananchi kujiunga na vyama hivi,sitakubali  kuona hali hii ikiendelea,”alisema.

Alisema Serikali inatambua ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa mtaji na kuwawezesha kuunganisha nguvu zao za kiuchumi katika kujiendeleza kiuchumi.

Alisema zipo juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanahamasishwa na hatimae kujiunga kwenye vyama vya ushirika kulingana na shughuli zao za kiuchumi ili kuondoa dhana kuwa vyama vya ushirika ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya biashara ya nchi za nje.

Tume

Aliitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Shirikisho la Vyama vya Ushirika kuendelea kuwahamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kujiunga katika vyama vya ushirika kulingana na shughuli zao.

Alisema wanaweza kujiunga kwenye ushirika wa viwanda, madini, ufugaji, usafirishaji, uvuvi na kilimo.

Alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa ushirika wa Taifa katika kuyafikia malengo ya milenia na malengo mbalimbali ya nchi kama uimarishwaji wa sekta ya viwanda, kilimo, uvuvi na biashara.

Kutokana na kazi nzuri anaoifanya, Julai, mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimkabidhi tuzo ya heshima Waziri Dk. Tizeba kwa kazi kubwa aliyoifanya na anayoendelea kuifanya katika kuimarisha sekta ya ushirika.

Moja ya hatua ambazo amekuwa akichukua ni pamoja na kuhusu ubadhilifu wa rasilimali za ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika.

Gharama

Kuhusu malalamiko ya muda mrefu ya wakulima yaliyokuwapo kwamba ushirika unatoa bei ndogo, Waziri Tizeba alisema sasa yamepatiwa muarobaini, baada ya Serikali kupitia kwa kina gharama za uendeshaji na uongezaji thamani kwa zao la kahawa kwa vyama vikuu vya ushirika mkoani Kagera.

“Serikali imepiga marufuku vyama vya ushirika kutoza zaidi ya shilingi 490 kwa kilo moja ya kahawa ya maganda kama gharama za uendeshaji na uongezaji thamani, mtakumbuka awali maainisho ya gharama hizi yalikuwa ni makubwa  mno hadi shilingi 1,350 kwa kilo moja ya kahawa ya maganda ilianishwa kama gharama za uendeshaji,”alisema.

Alisema amechukua uamuzi huo kutokana na kuwapo na malalamiko ya wadau wa kahawa ambapo gharama hizo zilionekana kuwa kubwa ukilinganisha na gharama halisi.

Alisema suala la ushirika, ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ndiyo mkataba kati ya wananchi na Serikali katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015-2020 inatoa maelekezo ya kuwezesha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo kwa kuviimarisha na kuviwezesha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na nje.

Aliaagiza wakulima waliouza kiasi kidogo cha kahawa wasilipwe kwa utaratibu wa benki ili kuepusha usumbufu, badala yake kwa wale wakulima waliolima hekari nyingi na malipo yao yatahusisha kiasi kikubwa cha fedha ndio walipwe hivyo.

 Agizo kwa CRDB

Aliitaka benki ya CRDB, kulipa haraka malipo ya fedha za Ushirika za Chama Kikuu cha Kagera (KCU) kulingana na hatma ya kesi iliyokuwa mahakamani mwaka 2003.

Alisema katika kesi hiyo, wakulima walikuwa wakikatwa Sh 10 kwa kila kilo moja ya kahawa ili kujenga mfuko wa mazao kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 1990 hadi 1993.

Suala la madai hayo, liliibuka baada ya baadhi ya wakulima kuonyesha vitabu vya mfuko huo ambapo makato hayo ya Sh 10 kwa kilo kwa kipindi cha miaka mitatu jinsi ambavyo yalikuwa yakifanyika.

Madai ya wakulima hao yamekuwa yakilalamikiwa kwa kipindi kirefu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa imani ya wakulima kwa (KCU).

Alisema hukumu ya kesi iliyotolewa Oktoba 28, 2009 na Mfuko wa Mazao ya Wakulima Mkoa wa Kagera kupewa tahfifu ulizoomba ambapo tangu wakati huo Benki ya CRDB iliweza kulipa fedha za mfuko ilizochukua Sh milioni 525.

Alisema madai hayo sambamba na riba, ni Sh bilioni 6, huku akisisitiza CRDB inapaswa kuwa mfano wa benki zingine kwa kulipa madeni.

Kagera Sugar

Akikagua kiwanda hicho, alikitaka kuachana na urasimu urasimu katika mfumo wa uuzaji wa sukari wanayozalisha, badala yake kuingiza mtaani kwa wingi ili wasipate  upungufu wa huduma hiyo.

“Natoa siku 14 kwa kiwanda hiki kuongeza kasi ya uzalishaji kutoka uzalishaji wa sukari  wa tani 350-360 kwa siku ili kufikia walau tani 450 hadi  500 kwa siku, kufanya hivi mtasaidia uwezo wa sukari kupatikana kwa wingi,”alisema.

Aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuongeza idadi ya mawakala haraka.

Utafiti

Katika ziara hiyo, alizungumza na uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Maruku, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) na kuwataka hao kuongeza ufanisi katika utaalamu wao ili kuwanufaisha wakulima.

Alisema wataalamu wa utafiti wanapaswa kufanya vizuri pia katika eneo la kutangaza tafiti zao, ikiwamo kuongeza ujuzi katika utafiti wa mazao mbalimbali.

Aliwasihi watafiti kuendelea kufanya juhudi kubwa kuandika miradi mbalimbali (Research Proposals) kwa ajili ya kusaidia shughuli za uendelezaji wa utafiti kwani bajeti ya serikali pekee haiwezi kutosha kukamilisha kila changamoto zinazowakabili.

Katika hatua nyingine, alimwagiza Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (Maruku), Laurent Mathew Luhembe ndani ya mwaka mmoja kutatua changamoto ya ukosefu wa bweni la chakula.

Waziri wa Uganda

Naye Waziri wa Biashara na Ushirika nchini Uganda, Fredric Ngobi Gume alisema si kweli kahawa inauzWa bei kubwa.

Alisema kilo moja ya maganda ya kahawa nchini Uganda, inanunuliwa Sh 2,000 za Uganda sawa na Sh 1,400 za Tanzania.

“Kwa mfano hapa Tanzania wiki iliyopita ambayo mnada wake umefanyika mjini Moshi, kilo iliuzwa wastani wa Shilingi 1,460 ya bei elekezi ya chini ya kila wiki (Indicative price) inayotolewa na Bodi ya Kahawa kulingana na bei ya Kahawa katika soko la dunia,”alisema.

“Ndugu zangu kuna jambo hamlifahamu wale wanaosema Uganda bei ya kahawa ni nzuri kuliko Tanzania, wanawadanganya hakuna bei nzuri kule kinachofanya watu kupeleka Uganda ni kutokana na mikopo wanayokopeshana isiyo rasmi (Butura).

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,587FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles