24.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 28, 2022

Contact us: [email protected]

TINGATINGA LA BOMOA BOMOA KIMARA LAISHIWA MAFUTA

CECILIA NGONYANI (Turdaco) Na TUNU NASSOR

-DAR ES SALAAM

TINGATINGA la Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, linalovunja nyumba zilizopo katika hifadhi ya barabara ya Morogoro, limeshindwa kuendelea na kazi baada ya kuishiwa mafuta.

Hali hiyo ilitokea jana saa saba na nusu mchana eneo la Kimara Stop Over wakati tingatinga hilo likiendelea na uvunjaji wa nyumba.

Bomoa bomoa hiyo ambayo imeanza kwa wiki ya tatu sasa, ikianzia Kiluvya, inatarajiwa kuzikumba nyumba zaidi ya 1,300 zilizopo mita 121.5 kutoka katikati ya barabara, zikiwamo za ibada, huduma za jamii na vituo vya mafuta.

Mmoja wa wafanyakazi wa Tanroad ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, aliliambia MTANZANIA kuwa tingatinga hilo liliishiwa mafuta baada ya kubomoa nyumba moja.

“Mtu ambaye anatakiwa kuongea na nyinyi ametoka hapa akisindikizwa na polisi kufuata mafuta baada ya mashine hii kuishiwa,” alisema huku akionyesha tingatinga hilo.

Wakati huohuo, mmoja wa wahanga wa bomoa bomoa hiyo, mkazi wa Kibamba CCM, Manyuka Ahmad, ameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuhamisha makaburi ya ndugu zake waliofariki dunia miaka mingi iliyopita.

“Hapa kuna makaburi ya marehemu waliofariki tangu 1999, waliokuwa wakiishi hapa, hivyo tunaiomba Serikali ituandalie utaratibu wa kuihamisha miili yao kabla ya kubomoa eneo hili,” alisema Ahmad.

Naye Nyahali Manyuka, alionekana kulia muda wote huku akisema hajui wapi pa kwenda kuizika mifupa ya dada yake na wanawe watakapofukuliwa kupisha upanuzi wa barabara.

“Inauma sana kuona watu tuliowazika miaka mingi wakiwa kamili, leo wanafukuliwa wakiwa mifupa tu, niacheni nilie kwa walichotufanyia,” alisema Nyakali.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibamba, Ally Kagombe (CCM), alisema si kweli kuwa bomoa bomoa hiyo imekuja bila taarifa kama wanavyosema baadhi ya waathirika.

“Jambo hili halikuwa na upendeleo wowote, hata ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Kata ya Kibamba imebomolewa na hakuna aliyelalamika, maendeleo yanapokuja yana maumivu yake, hivyo niwatake wananchi wenzangu kuwa wavumilivu,” alisema Kagombe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,405FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles