24.3 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Timu ya Wanasheria yaambatana na Rais Samia ziara ya Morogoro

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

TIMU ya wanasheria wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid imeambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake mkoani Morogoro kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Rais Samia yuko katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro iliyoanza tarehe 2 na inayotarajiwa kukamilika  Agosti 7, 2024.

Akizungumza Agosti 2, 2024, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo, alisema wameambatana na Rais Samia ili kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria.

“Tutakuwa na Rais muda wote wa ziara hapa Morogoro na tuko na Waziri wetu Mheshimiwa Pindi Chana na wasaidizi wa kisheria ngazi ya wilaya na mkoa. Kila anapofika Mheshimiwa Rais, kama kuna mtu ana changamoto ya kisheria, tunaichukua na kuifanyia kazi.

“Kupitia ziara hii, tumeshatoa msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali na hata jamii ya Wamasai. Tumekutana nao kwenye maeneo mbalimbali na kuwapa elimu ya sheria kuhusu migogoro yao ya mara kwa mara ya ardhi,” alisema Beatrice.

Beatrice alisema wakati wanasheria wengine wakiwa kwenye ziara hiyo, Rais Samia ametuma wanasheria wengine kupitia Kampeni ya Mama Samia Legal Aid kutoa huduma za msaada wa kisheria kwenye maonyesho ya Nanenane mkoani humo.

Timu ya wanasheria hao iliwasili mkoani Morogoro juzi na inaendelea kuwahudumia wananchi mbalimbali wenye matatizo ya kisheria kwa kuwapa msaada.

Tangu wanasheria hao wawasili kwenye viwanja vya Nanenane mkoani Morogoro, wananchi wengi wamekuwa wakifika kwenye banda la Mama Samia Legal Aid na kupokea msaada wa kisheria.

Mama Samia yuko mkoani hapo kwa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya za Mkoa wa Morogoro. Mpaka sasa ameshatembelea Wilaya ya Gairo, Kilosa, na Mvomero, na kesho Jumapili anatarajiwa kuwasili Wilaya ya Kilombero.

Mmoja wa wananchi waliopata huduma ya msaada wa kisheria, Jerome Kiangi, alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kutatua matatizo yao ya kisheria.

“Kwa kweli nampongeza Rais Samia kwa upendo wake kwa Watanzania. Amebaini kwamba wengi wetu tunahitaji msaada wa kisheria. Nimekuja hapa na kusikilizwa na wanasheria ambao wamesema tatizo langu la mgogoro wa nyumba litapatiwa ufumbuzi. Namshukuru sana,” alisema Kiangi.

Mwananchi mwingine, John Lubeja, alipongeza hatua ya Rais Samia kutuma wanasheria kwenye maonyesho hayo, akisema wamekuwa mkombozi kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kupata huduma za kisheria.

“Kupata wakili ni gharama sana. Kwa hiyo huduma kama hizi zinaposogezwa karibu na wananchi kama hapa kwenye maonyesho, tena bure, ni jambo la faraja sana na la kupongeza mno,” alisema Lubeja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles