24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

TIDO MHANDO AKUTWA NA KESI YA KUJIBU

Na KULWA MZEE-DAR EA SALAAM


ALIYEKUWA  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando anayekabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka akutwa na kesi ya kujibu.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifikia uamuzi huo jana baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali kutoka TAKUKURU, Leonard Swai kufunga ushahidi kwa mashahidi watano.

Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi mahakama ilimuoma Tido ana kesi ya kujibu dhidi ya mashtaka yanayomkabili hivyo kuamuru aanze kujitetea Septemba 29 mwaka huu.

Tido anawakilishwa mahakamani na Wakili Dk.  Ramadhani Maleta na Martine Matunda.

Awali aliposomewa maelezo ya awali, Tido alikubali maelezo yake binafsi, alikubali alikuwa Mkurugenzi  Mkuu wa TBC  mwaka 2006 hadi 2010.

Mshtakiwa huyo alikubali alikuwa msimamizi katika shughuli za TBC lakini  siyo kwa shughuli zote.

Tido alikubali kutoa maelezo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) lakini alikana mashtaka yote yanayomkabili.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 887.1.

Inadaiwa kuwa Juni 16, 2008 akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Ununuzi na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi,  kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa  Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho  anadaiwa  kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh 887,122,219.19.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles