24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

TIC yasajili miradi ya dola bilioni 20 kwa miaka minne

TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

KITUO cha Uwekezaji (TIC) kimefanikiwa kusajili miradi 1,312 katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2020 ambayo inakadiriwa kuwakeza kiasi cha mtaji wa Dola za Marekani bilioni 20.427.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe alisema miradi hiyo inatarajia kutoa fursa za ajira kwa Watanzania wapatao 178,101.

Alisema sekta ya viwanda ndiyo inayoongoza katika uwekezaji ambayo imechukua asilimia 54 ya miradi yote na kutoa ajira kwa Watanzania 67,992 huku mtaji uliowekezwa ni Dola za Marekani milioni 4.710.

“Uwekezaji huu wa viwanda unakwenda sambamba na malengo ya utekelezaji wa Ilani ya chama tawala ambayo ilijipambanua katika kujenga uchumi wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati,” alisema Mwambe.

Alisema katika miradi hiyo, ya wazawa ilikuwa 365 ikiwa sawa na asilimia 28, wageni 571 sawa na asilimia 43 na ya ubia kati ya wazawa na wageni ni 376.

Mwambe alisema sekta ya kilimo ilikuwa na miradi 85 ambayo ilikuwa na mitaji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 7.983 huku ikitoa ajira kwa Watanzania 54,526.

Alisema sekta ya tatu iliyofanya vizuri ni nishati ambayo ilikuwa na miradi 22 iliyokuwa na mtaji wa Dola za Marekani bilioni 3.225 na ikizalisha ajira 1,416.

Akizungumzia  mafanikio mengine, Mwambe alisema wamefanikiwa kuanzisha Kamati ya Taifa ya Uwezeshaji Uwekezaji (NIPC) iliyoundwa na wakuu wa taasisi zinazotoa vibali kwa wawekezaji.

“Lengo la kamati hii ni kuwa na mkakati wa pamoja kusaidia kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji katika maeneo wanayoyasimamia,” alisema Mwambe.

Alisema katika kipindi hicho, kituo hicho kimeimarisha mifumo ya utoaji vyeti, vibali vya makazi na rufaa ikiwa ni pamoja na kuunganisha mifumo mingine ya Serikali.

Akizungumzia sheria na sera, Mwambe alisema kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu wameanzisha mchakato wa kuzihuisha ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji .

“Rasimu ya sheria imekamilika, wadau wametoa maoni yao na sasa ipo katika hatua za Serikali kuikamilisha na naamini katika Bunge lijalo tutapata sheria mpya,” alisema Mwambe.

Alisema katika kuhakikisha wanawafikia wananchi wengi, wameongeza ofisi za kanda za kituo hicho kutoka tatu na kufikia saba na kuboresha huduma za mahala pamoja (one stop facilitation centre) huku taasisi zikiongezeka kutoka saba na kufikia 10.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,249FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles