Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema zaidi ya asilimia 90 ya dawa za asili zilizofanyiwa uchunguzi kuhusu uwezo wake wa kutibu maradhi mbalimbali zimegundulika kuwa na kemikali zenye sumu ambazo ni hatari kwa binadamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema aina ya kemikali zenye sumu zilizogundulika kuwa kwenye dawa hizo ni pamoja na Alkaloid, Saponin na Anthroquinone.
Waziri Mwalimu alisema taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali mwaka 2015/16, imeonyesha kuwa kati ya aina 95 za dawa zilizopokelewa na kufanyiwa vipimo ni asilimia saba pekee ndiyo iliyogundulika kuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
“Ofisi ya Mkemia Mkuu ilipima aina 95 ya dawa hizo, asilimia saba tu ndizo hazikuwa na kemikali zenye sumu lakini kiasi kilichobaki kilikuwa na sumu lakini tunaona waganga hao hasa wa mijini wanaendelea kuzitumia kwa kuwapa wananchi jambo ambalo ni hatari,” alisema Waziri Mwalimu.
Alisema uchunguzi huo pia ulibaini kuwapo kwa kasoro nyingi kuhusu matumizi ya tiba za asili na kwamba waganga wengi hawajasajiliwa na Baraza la Tiba za Asili Tanzania.
“Katika uchunguzi wa ofisi ya mkemia mkuu ilibainika kuwa vifaa vinavyotumiwa na waganga wa kienyeji kupima magonjwa havijasajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora (TBS) na dawa zao hazijasajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA).
“Baada ya tamko la awali tuliwaita waje kujisajili lakini ni 28 tu ndio walioleta majina na nyaraka zao ambapo watano walikuwa na vibali vya matangazo, watano hawakuwa navyo lakini walikuwa wakirusha matangazo yao hewana na wengine 18 hawakuwa na matangazo kabisa,” alisema Waziri Mwalimu.
Alisema kasoro hizo zilibainika baada ya ziara ya kushtukiza ya naibu wake, Dk. Khamis Kigwangwala aliyoifanya Desemba 14, mwaka jana katika kituo cha tiba asili cha Fore Plan Clinic kinachomilikiwa na Tabibu Juma Mwaka.
“Ni marufuku kwa mtu yeyote kutoa huduma hizo bila kusajiliwa, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lihakikishe sheria zinafuatwa ili waganga wa asili wote wasajiliwe kwa wale walioko mijini usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi mitatu na wale wa vijijini, usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi sita.
“Vifaa vyote ambavyo havijasajiliwa navyo ni marufuku, watu wangu wataingia mtaani tunavikamata na hatuna mzaha katika hili sababu tunalinda maisha ya Watanzania, nenda TFDA na wao nawaagiza ndani ya siku saba hadi 14 watoe vibali,” alisema Waziri Mwalimu.
Sambamba na hilo, pia alipiga marufuku ugawaji na uuzwaji wa dawa yoyote ile ya tiba asili hadi isajiliwe na kuwa imechunguzwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa matumuzi ya binadamu na kwamba ni lazima pia iwe na kibali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
“Ni marufuku pia kuendesha kituo cha kutolea huduma za tiba pamoja na kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kuhusu tiba asili na tiba mbadala.
“Lakini agizo hili haliwahusu sana wale wa vijijini kwa sababu hawajitangazi na wanatibu magonjwa kwa dawa za asili na hiyo inakubalika tangu zamani, sheria haimtaki kusajili dawa yake lakini wale wanaosema kwamba dawa zao zinatibu uvimbe watu wanapata ujauzito hizo ndiyo tunataka wazisajili,” alisema Waziri Mwalimu.
Naye Naibu Waziri, Dk. Kigwangwala alisema alisoma nyaraka zote zilizowasilishwa na waganga hao na kubaini kwamba wote hawakuwa halali.
“Hata Juma Mwaka alikuwa na nyaraka za kituo chake na zake binafsi na wasaidizi saba hakukuwa na hata mmoja aliyesajiliwa, hii si sahihi kwa mujibu wa sheria ya 2002.
“Dk. Mwaka alipaswa kufungiwa moja kwa moja, lakini tumeona tutoe muda kidogo wa watu kujiweka sawa kabla hatujaanza kuwashughulikia, hatutakuwa na msalia Mtume tukipita tutafunga,” alisema Naibu Waziri Kigwangala.