27.2 C
Dar es Salaam
Monday, January 20, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

THRDC yasisitiza mazingira salama kwa watetezi wa haki za watu wenye ulemavu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Dawati la Watetezi Wenye Ulemavu kupitia Mtandao wa Watetezi wa Haki za Watu Tanzania (THRDC) linakusudia kuweka mazingira salama, jumuishi na wezeshi kwa Watetezi wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (HRDDs).

Mkuu wa Dawati la Watetezi Wenye Ulemavu, Emmanuel Majeshi, amesema lengo ni kuimarisha msaada na ulinzi wao wa kisheria, ki-taasisi, kifedha, kijamii na kiteknolojia.

Majeshi ameeleza hayo kupitia tamko lake kuhusu maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani.

Amesema dawati hilo pia linalenga kuboresha uwezo wa taasisi za watetezi wa haki za Watu wenye ulemavu na taasisi zinazowaunga mkono kwa kuongeza ujuzi na maarifa yao kupitia programu maalum za mafunzo.

“Dawati linalenga kuongeza uelewa kwa umma kuhusu kazi muhimu za watetezi wa haki za Watu wenye ulemavu na kuanzisha majukwaa ya kupaza sauti zao.

“Tunasimama bega kwa bega na watetezi wa haki za Watu wenye ulemavu na kutambua mchango wao muhimu katika utetezi wa haki za watu licha ya changamoto nyingi wanazokutana nazo. Watu wenye ulemavu hasa watetezi wa haki za watu wenye ulemavu bado wanapitia madhira mbalimbali kama ubaguzi na unyanyasaji,” amesema Majeshi.

Kulingana na utafiti wa mahitaji uliofanywa na THRDC mwaka 2023 kwa ajili ya Watetezi wa Haki za Watu wenye Ulemavu (HRDDs) nchini, ulibainisha changamoto kadhaa kwa Vyama/Taasisi za Watu Wenye Ulemavu (OPDs).

Changamoto hizo ni pamoja na taasisi nyingi kutokuwa na uwazi na mgawanyo ya majukumu, kujihusisha na siasa na ukosefu wa mafunzo ya uongozi.

“Taasisi nyingi za watu wenye ulemavu hazihusiki kikamilifu katika majukwaa ya uchechemuzi wa haki za watu wenye ulemavu, kuna upungufu wa usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi ndani ya taasisi hizo,” amesema.

Aidha amesema ripoti ya utafiti wa tathmini ya mahitaji ilichangia kwa kiasi kikubwa kuanzishwa kwa Dawati la Watetezi wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (DDI) lililo chini ya TRHDC.

Amesema matukio ya hivi karibuni dhidi ya watu wenye ualbino kama mashambulizi ya kikatili dhidi ya Kazungu Julius huko Katoro – Geita na mauaji ya Asimwe Novath huko Muleba – Kagera ni mfano wa mazingira hatarishi ambayo watu wenye ulemavu hasa wenye ualbino wanakutana nayo katika jamii.

Amesema matukio hayo yanachangiwa na dhana potofu katika jamii dhidi ya viungo vya mtu mwenye ualbino katika kujipatia utajiri na nafasi za uongozi, na kwamba mara kadhaa matukio hayo yameshuhudiwa zaidi kipindi cha uchaguzi.

Amesema kuna uhitaji wa ulinzi zaidi, mabadiliko ya sera na kujenga uelewa kwa jamii juu ya mtazamo sahihi dhidi ya watu wenye ulemavu kwa kuwapa nafasi katika jamii pasipo kuzingatia utofauti.

Amesisitiza kupaza sauti za watu wenye ulemavu kuhakikisha ushiriki wao wa moja kwa moja katika ujenzi wa mustakabali jumuishi na kuwawajibisha wale wanaovunja haki zao.

Amesema uongozi wa watu wenye ulemavu ni muhimu katika kujenga jamii endelevu ambapo kila mtu bila kujali uwezo wake, anapata nafasi ya kuchangia na kustawi.

“Tunaendelea kufanya uchechemuzi wa sera zinazokuza ujumuishwaji na ulinzi wa watu wenye ulemavu na kuhakikisha kuwa watetezi wa haki za watu wenye ulemavu (HRDDs) wanapata rasilimali na msaada wa kutosha ili kutekeleza kazi zao muhimu.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau wengine ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu wenyewe kujenga jamii inayoheshimu haki za watu na kuthamini uongozi na hadhi ya watu wenye ulemavu,” amesema.

Ametoa wito kwa Watanzania, taasisi za serikali, asasi za kiraia kuungana katika kulinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema; ‘Kukuza Uongozi wa Watu Wenye Ulemavu kwa Maendeleo Endelevu na Jumuishi,”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles