Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wenye mashirika wanachama zaidi ya 300 hapa nchini umesema kusitishwa kwa miradi na fedha za Marekani ni pigo kubwa kwa sekta ya AZAKI na kwa Watanzania.
Tayari mtandao huo umefanya utafiti kufuatia uamuzi huo na kubaini kuwa kusitishwa ghafla kwa ufadhili wa Marekani kumesababisha madhara makubwa kwa mashirika yaliyopewa taarifa rasmi za kusimamisha miradi yote inayotegemea fedha za Marekani.
Mratibu Taifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema leo Februari 10,2025 wanaoathirika zaidi ni wanufaika wa miradi hiyo inayogusa maisha ya Watanzania wengi.
“Uamuzi huu wa Serikali ya Marekani umetoa somo muhimu kwa sekta ya asasi za kiraia nchini umuhimu wa kujenga mifumo ya kifedha iliyo imara na kupunguza utegemezi wa misaada ya nje,” amesema Wakili Olengurumwa.
Aidha amesema ili mashirika ya kiraia yaweze kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kujikwamua na changamoto hiyo ni muhimu kuimarisha mashirika ya ndani kwa kuweka sera na mikakati ya kupata ufadhili wa moja kwa moja.
“Kumekuwa na changamoto ya muda mrefu kwa sera za nchi yetu kuruhusu mashirika ya kigeni kusajiliwa kama mashirika ya wazawa hali inayozidi kudhoofisha mashirika ya ndani, mashirika ya kigeni hufanya utekelezaji wa miradi moja kwa moja kwenye jamii na jamii kujenga hali ya utegemezi katika mashirika hayo.
“Inapotokea mabadiliko ya kisiasa na sera kwenye nchi zao, na wanapoamua kufunga huduma zao, panakuwa hakuna tena mikakati ya uendelevu wa huduma nchini na kupelekea madhara makubwa kama ilivyo sasa,” amesema.
Amesema ni wakati wa serikali na watunga sera kuangalia suala hilo kwa mapana na kuchukua hatua sitahiki za kuhakikisha mashirika ya ndani yanaimarika kwa kushiriki moja kwa moja ktika utekelezaji wa miradi hiyo katika maeno yao kuliko kusubiri kushirikishwa katika gawio la ruzuku ndogo.
Mratibu huyo wa THRDC pia amependekeza mashirika kushirikiana na wafanyabiashara, taasisi za kifedha na wahisani wa ndani ili kuongeza vyanzo vya fedha kwa ajili ya miradi yao.
Mashirika hayo yalikuwa yanatoa ajira kwa maelfu ya Watanzania, yanaendesha miradi katika afua mbalimbali za maendeleo hapa nchini zikiwemo, afya, elimu, demokrasia, mazingira, kilimo, maji, vijana, wanawake, amani na mengine.
Kuathirika kwa mashirika hayo kumeathiri pia ufanisi wa mashirika ya wazawa yaliyokuwa yanafanya kazi kwa ushirika au kutoa ruzuku kwa mashirika ya wazawa.