Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Serikali imeshauriwa kupanga mikakati mipya ili kuwezesha wanawake na makundi mengine yaliyoko pembezoni kushiriki katika maendeleo ya taifa ambayo ni jumuishi na endelevu.
Akizungumza leo Machi 6,2024 Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) Lilian Liundi, amesema licha ya Serikali kuonyesha dhamira ya kuongeza usawa wa kijinsia lakini bado kuna changamoto nyingi.
Liundi alikuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake yaliyofanyika katika viwanja vya TGNP Mabibo na kushirikisha makundi mbalimbali ya wanawake na wadau wa maendeleo.
“Safari ya kufikia usawa wa kijinsia maendeleo endelevu na jumuishi inahitaji kutafakari na kupanga mikakati mipya ili kuwa na jamii yenye usawa.
“Bado kuna changamoto nyingi zinazowakwamisha wanawake na makundi mengine yaliyoko pembezoni kushiriki katika maendeleo ya taifa ambayo ni jumuishi na endelevu,” amesema Liundi.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi za uongozi na kutoa maamuzi, mila kandamizi desturi na mitazamo hasi dhidi ya wanawake, kukosekana kwa mifumo rasmi na wezeshi ya kikatiba, kisheria na kisera na ukatili wa kijinsia hasa rushwa ya ngono.
Liundi ametoa mfano wa idadi ya wabunge wanawake ambao ni 141 (asilimia 37) kati ya wabunge wote 393 kwamba bado ni ndogo kulinganisha na lengo la kufikia asilimia 50 kwa 50.
Naye Mratibu wa Masuala ya Jinsia wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women), Karen Giath, amesema miswada ya sheria za uchaguzi iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge itaongeza ushiriki wa wanawake na kuwapa nguvu ya kushiriki katika uchaguzi.
Aidha amesema mwaka huu wanawake bilioni 2 katika nchi 15 ikiwemo Tanzania watafanya uchaguzi na kutaka waungwe mkono kuongeza ushiriki wao katika ngazi za maamuzi na kuhakikisha lengo namba tano la maendeleo endelevu linafakiwa.
Mchambuzi Mwandamizi wa Mipango kutoka Ubalozi wa Canada, Taslim Madhani, amesema Tanzania imepiga hatua katika usawa wa kijinsia hasa katika masuala ya elimu, uongozi na maamuzi lakini bado kuna kikwazo katika kufikia usawa wa kweli.
“Lazima tuwawezeshe wanawake na mabinti, tuendelee kupigania kesho tunayoitaka kwa mama zetu na mabinti zetu,” amesema Madhani.