25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

TFS yaanza maboresho hifadhi ya msitu Mazingara huku watalii wakiongezeka

Na Mwandishio Wetu, Mtanzania Digital

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki wameanza kuboresha huduma za utalii katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira wa Vikindu uliopo wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Katika mahojiano na Mtanzania Digital yaliyofanyika juzi mkoani Pwani, Meneja wa TFS Kanda ya Mashariki, Caroline Malundo, amesema kuwa ofisi hiyo imekuwa ikisafisha njia za asili, kujenga vyoo na kununua mahema kwa ajili ya watalii hao ikiwa ni sehemu ya mipango hiyo.

Aidha, amesema maendeleo hayo mapya yanakuja kutokana na msitu huo kuona ongezeko la watalii wanaotembelea eneo hilo na kuongeza kuwa hifadhi ya Misitu hiyo ni miongoni mwa misitu iliyo nusu ya mijini nchini, iliyoko kilomita 17 kutoka Jiji la Dar es Salaam. Msitu huo ambao ni miongoni mwa misitu mitatu inayounda Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Pugu Kazimzumbwi (mengine ni Pugu na Kazimzumbwi) unatoa mahali pazuri kwa watu wanaotafuta utulivu nyikani.

“Mbali na hayo, tuko katika harakati za kushirikiana na wawekezaji katika kuendeleza shughuli za utalii katika msitu huu. Tayari tumepokea maombi kutoka kwa baadhi ya wadau na hadi sasa mchakato unaendelea vizuri,” amesema Malundo nakuongeza kuwa moja ya vipaumbele katika mwaka ujao wa fedha itakuwa kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha barabara za kuingia ndani na kuzunguka msitu.

Amesema ndani ya msitu huo kuna vivutio vingi vya utalii ambavyo ni pamoja na mabwawa mawili ya asili, aina 65 za miti ya asili ikiwemo Mkangazi, Mswe na Mzambarau, daraja la miti lenye urefu wa mita 52 na wanyama wadogo kama nyani, nyani blue, nguruwe pori, aina mbalimbali za ndege na idadi kubwa ya panzi wazuri.
Ikumbukwe kuwa pori hilo lilipandishwa hadhi na kuwa Hifadhi ya Mazingira mwaka 2020.

Kwa upande wake, Mhifadhi Msitu wa Wilaya ya Mkuranga (DFC), Charles Kuselya, alisema idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka tangu msitu huo upandishwe hadhi mwaka juzi.

“Idadi ya watalii wanaotembelea tovuti yetu imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku. Kwa mfano katika kipindi cha miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba 2021, jumla ya watalii 300 walitembelea tovuti yetu, mwezi Oktoba pekee tulipokea jumla ya watalii 400. Hii inaonyesha kuwa watu zaidi wanavutiwa na msitu wetu na wengi wao wakiwa watalii wa ndani,” anasema Kuselya.

Pori la Vikindu lina ukubwa wa hekta 1,690 na limezungukwa na vijiji saba vya Mwandege, Kipala Mpakani, Mlamleni, Kisemvule, Luzando, Vikindu na Picha ya Ndege.

Msitu huo ulikuwa ukikabiliwa na vitendo vya uvamizi mkubwa katika miaka ya nyuma na hivyo kusababisha uharibifu wa mimea yake kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, kufuatia hatua kali za ulinzi na uhifadhi wa TFS na wadau wake, sasa imerejea katika hali yake ya zamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles