TFF MMEAMUA KUWA MATAPELI?

0
1691

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


tffWIKI iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kuvunja mkataba wa aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa (Taifa Stars), Boniface Mkwassa

Sababu kubwa iliyotajwa katika uamuzi huo ni muda, yaani TFF iliona kwamba kwa sasa hawana shida na Mkwassa hivyo wakaamua kumtimua.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas anasema kuwa wamefanya uamuzi huo, huku wakiwa hawana deni zaidi ya fidia ya muda uliobakia kwa kocha huyo.

Mkwassa alitakiwa kumaliza mkataba wake Machi mwaka huu, hivyo TFF watalazimika kumlipa fidia kwa hawamu mbili yaani Januari na Machi.

Mbali na fidia hiyo, lakini Mkwassa bado anaidai TFF, licha ya TFF kudai wamemalizana na kocha huyo.

Kutokana na madai ya mshahara wa miezi mitatu, kuna wakati Mkwassa alidaiwa kuweka ngumu kuendelea kuifundisha timu hiyo.

Kipindi hicho  alihusishwa kurejea kuifundisha timu yake ya zamani Yanga, lakini suala hilo lilizimwa, baada ya TFF kupunguza deni hilo na kubaki miezi miwili.

Licha ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi kutangaza kulipa deni la mshahara wa kocha, Mkwassa, ilielezwa kuwa mshahara ulikuwa ukilipasua kichwa shirikisho, hilo kutokana na ukubwa wake.

Ukubwa wa mshahara wa kocha, huyo ulikuwa ukigharimu zaidi ya nusu ya mishahara ya wafanyakazi wa TFF, ambapo awali ulikuwa ukilipwa na serikali.

Kocha huyo inadaiwa alikuwa akipokea kwa mwezi kiasi cha Shilingi milioni 28 mshahara, aliourithi kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Martin Nooij ambaye naye aliurithi kutoka kwa Mbrazili, Marcio Maximo.

Mishahara hiyo  ilikuwa ikilipwa na serikali ya awamu ya nne, hivyo kulifanya sasa shirikisho hilo kuwa na mzigo mkubwa katika suala zima la kulipa mshahara huo.

Oktoba mwaka jana Malinzi alikiri kuhusu kudaiwa mshahara na Mkwassa, ambapo aliahidi kutekeleza jukumu hilo ndani ya mwezi huo.

Lakini kinachoshangaza ni kuona sasa wakilikimbia deni hilo na kudai kwamba wameshamalizana wakati Mkwassa akitamka adharani kuwa bado analidai shirikisho hilo.

Mkwasa anasema:“Kuepusha migogoro isiyokuwa na maana ningependa TFF wanilipe fedha zangu mbali na hizo wanazodai kuwa ni fidia za muda wa mkataba wangu.”

Kwa haraka haraka hapa TFF, wanajaribu kukwepa ukweli kwamba wanadaiwa na wanatakiwa kulipa deni hilo licha ya kuwa kubwa.

Litakuwa jambo la aibu na fedheha kwa TFF, kama wakishindwa kumlipa Mkwassa kutokana na kazi aliyofanya akiwa kocha wa timu ya taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here