NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa, anatarajia kuongozana na mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta, kuelekea kwenye sherehe za utoaji wa tuzo kwa wachezaji bora barani Afrika nchini Nigeria.
Samatta ambaye anakipiga katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, anawania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Baraka Kizuguto, imeeleza kuwa Mwesigwa ataondoka na Samatta leo kuelekea Mji wa Abuja, Nigeria ambako tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa kesho.
Imeelezwa kuwa katika sherehe hizo Mwesigwa ataambatana na Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria.
Samatta pia ni mfungaji bora wa michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuifungia klabu yake ya TP Mazembe mabao saba yaliyosaidia timu yake kuibuka mabingwa akilingana na mshambuliaji wa El-Mereikh ya Sudan, Bakri Al-Madina.
Katika kinyang’anyiro cha tuzo ya mchezaji bora wa Afrika, Samatta atachuana vikali na mlinda mlango wa TP Mazembe, Robert Kidiaba ambaye ni raia wa Congo DR na mshambuliaji wa Etoile du Sahel, Baghdad Boundjah raia wa Algeria.
Kama Samatta akifanikiwa kuibuka mshindi kwenye tuzo hiyo, ataweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo hiyo katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ambayo pia itamsafishia njia kwenye mipango yake ya kwenda kucheza soka barani Ulaya.
Hata hivyo, tayari mshambuliaji huyo anayemaliza mkataba wake katika timu ya TP Mazembe amepata dili la kwenda kuichezea klabu ya KRC Genk ya Uturuki, ambayo anadaiwa atajiunga nayo baada ya sherehe hizo kumalizika.
Wakati huo huo Rais wa TFF, Jamal Malinzi, amemtakia kila la kheri Samatta kwenye kinyang’anyiro hicho kwa niaba ya Watanzania wote, ili aweze kuibuka mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.