25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

TFDA YAWAFUNDA WASINDIKAJI  VYAKULA

Na MASYENENE DAMIAN-MWANZA


MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Ziwa, imewafunda wajasiriamali wanaojihusisha na biashara ya usindikaji, uzalishaji wa chakula jijini Mwanza, ili kutatua changamoto ya ubora na usalama wa chakula nchini.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalilenga kuwasaidia wajasiriamali hao kuzijua sheria, kanuni na miongozo ya usindikaji, uzalishaji wa chakula kilicho salama na bora.

Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu kutoka TFDA, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (Sido) na sekta ya afya mkoani Mwanza.

 

Wakizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili, wasindikaji hao waliziomba mamlaka husika za Serikali kuweka mazingira rafiki katika sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kuondoa urasimu katika kusajili bidhaa na majengo, mitaji na mikopo katika taasisi za fedha.

Mmoja wa wasindikaji wa pilipili na unga wa lishe, Victoria Gachocha, alisema wanalazimika kununua vifungashio vya bidhaa zao kutoka nje ya nchi kwa sababu vya ndani havina ubora na vinapatikana kwa gharama kubwa.

Alisema upatikanaji wa vifungashio vilivyo bora, kutengewa maeneo ya usindikaji,  gharama kubwa za usajili wa bidhaa na kulindwa kwa haki za wabunifu wa bidhaa hizo, bado ni changamoto kwao hivyo aliiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ili waweze kuzalisha kwa tija zaidi.

 

Msindikaji wa vinywaji, Mkishage Julius, alilalamikia ugumu wa kupima ubora wa bidhaa hiyo ambapo sampuli zake hulazimika kupelekwa jijini Dar es Salaam kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, hivyo aliomba huduma hiyo isogezwe karibu na watumiaji.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza upande wa uchumi na uzalishaji, Johansen Kwayu, aliwahimiza wasindikaji hao wadogo kuwashirikisha wataalamu wa mamlaka hizo katika uzalishaji wa bidhaa zao.

“Ubora na usalama wa chakula ni sharti muhimu kwa wateja tunaowalenga na kutusaidia kudumu katika biashara tunayoifanya,” alisema.

Mwezeshaji wa semina hiyo kutoka TFDA, Lazaro Mwangole, alisema bidhaa nyingi zinazoletwa na wasindikaji kusajiliwa hazina ubora na hazikidhi viwango kwa sababu hawajui taratibu za kufuata.

“Maelezo mengi yanayowekwa kwenye vifungashio yanapotosha, wengi wanaigana tu kwa sababu bidhaa zinafanana, kuna tatizo la usafi katika sehemu za kusindika vyakula na ukadiriaji wa muda wa matumizi ya bidhaa, hivyo tunapenda kuona wasindikaji wote wanazalisha bidhaa kulingana na sheria na viwango vilivyopo,” alisema.

Ofisa Biashara wa Sido Mkoa wa Mwanza, Maneno Maporo, alisema wanaendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa vifungashio ambapo wameendelea kuvinunua kwa wingi kutoka viwanda vikubwa na kuviuza kwa bei nafuu kwa wajasiriamali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles