LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
MAMALAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imesema inafuatilia taarifa za kuwapo pipi zinazodaiwa kuchanganywa na dawa za kulevya na kusambazwa maeneo mbalimbali nchini, hususan shuleni.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza, alipozungumza na gazeti hili.
Gaudensia alisema pipi kama zilivyo bidhaa nyingine za chakula ili iingizwe sokoni, ni lazima ziwe zimesajiliwa na mamlaka hiyo.
“Taarifa hizo tumezipata na tunaendelea kufuatilia kwa sababu pipi ni bidhaa ya chakula kama bidhaa nyingine ambazo hadi ziingizwe sokoni ni lazima zisajiliwe.
“Lakini hadi sasa hatujui ni pipi gani ambazo zinadaiwa kuwa na dawa za kulevya kwa sababu hadi sasa hatujaziona.
“Labda wenzetu kwa sababu mlikuwapo kwenye mkutano ambao walitangaza kuwapo pipi hizo mngetusaidia kutuonyesha ili tuzifahamu.
“Hatuwezi kupata taarifa tukashindwa kuzishughulikia kwa hiyo tunaendela kufuatilia,” alisema Gaudensia.
Kauli hiyo ya TFDA imetolewa siku chache tangu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Rogers Siyanga, alipodai kuwapo pipi ambazo zinadaiwa kuchanganywa na dawa za kulevya na kusambazwa na kuwauzia wanafunzi kuanzia awali hadi sekondari.
Ofisa wa mamlaka hiyo anayeshughulika na uchunguzi wa dawa hizo katika maeneo ya shule mbalimbali alidai pipi hizo zinauzwa kati ya Sh 100 na Sh 200.
Ofisa huyo ambaye jina lake halikutajwa kwa sababu za usalama, alidai watumiaji wakubwa wa pipi hizo ni wanafunzi kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea, ambao walikutwa wakizinunua na kula, bila ya kujua madhara yake.
Baadhi ya shule ambako pipi hizo zinadaiwa kuuzwa ni pamoja na za kata za Buza, Ukonga, Kigogo, Mbagala na Gongo la Mboto ambako idadi kubwa ya wafanyabiashara huzinunua katika maduka makubwa na kwenda kuuza shuleni.
Ofisa huyo alisema katika kila kata, shule nne zilikuwa na pipi hizo na kwamba waliwahoji baadhi ya wanafunzi na kuchukua vipimo kujua kiwango cha madhara waliyopata.
Alisema baadhi ya wanafunzi waliotumia pipi hizo zilisababisha waanze kutumia dawa za kulevya.
Miongoni mwa wanafunzi wanaotajwa kuathirika na utumiaji wa pipi hizo ni pamoja na mwanafunzi mwenye umri wa miaka 11 (jina tunalihifadhi) mkazi wa Mwananyamala, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Inaenezwa kuwa mwanafunzi huyo kwa sasa anatumia dawa hizo kwa kujidunga na sindano na kwamba amekwisha kuathirika na dawa hizo kiasi cha kupoteza mwelekeo na kufanya vitu visivyoeleweka.
Tatizo jingine la utumiaji wa mihadarati ambako lilibainika katika Shule ya Sekondari Juhudi iliyopo Gongo la Mboto, Manispaa ya Ilala idadi kubwa ya wanafunzi wameathirika na matumizi ya aina mbalimbali za dawa za kulevya ikiwamo bangi, mirungi, shisha na heroin.
Inadaiwa wanafunzi shuleni hapo wamefikia hatua ya kufanya vurugu na kuwapiga walimu wao kutokana na mfumo wao wa ubongo kuathirika na dawa hizo hali iliyosababisha kujikuta kufanya vitu vya ajabu.
Inaelezwa hali hali hiyo iliwalazimu kuzungumza na uongozi wa shule na kuomba msaada kambi ya jeshi iliyopo karibu na shule hiyo kupata ulinzi wa askari ambao hufika shuleni hapo kila siku asubuhi kuangalia usalama.
MTANZANIA LAPIGA KAMBI SHULENI
MTANZANIA jana lilifika shuleni hapo mapema asubuhi na kuweka kambi kwa muda kubaini ukweli wa jambo hilo.
Akiwa shuleni hapo mwandishi alishuhudia Polisi Jeshi (MP) mmoja (jina linahifadhiwa) akiwa anaendelea kuangalia hali ya usalama shuleni hapo ikiwamo kuhakikisha hali ya utulivu miongoni mwa wanafunzi.
Kwa muda wote huo polisi jeshi huyo alikuwa akizunguka katika mazingira ya shule hiyo akiwa ameshika fimbo ndogo huku akiwaamuru wanafunzi waliokuwa wakionekana kutoka nje ya vyumba vya madarasa ovyo kurejea madarasani.
Mmoja wa kina mama wanaouza sambusa katika shule hiyo alilieleza MTANZANIA kuwa askari hao wamekuwa wakienda shuleni hapo kwa karibu mwaka mmoja sasa ingawa hakufahamu kama wanakwenda kukabiliana na wanafunzi wakorofi.
“Ni kweli askari wapo tena ni MP (military police), wanakuja kila siku asubuhi wanazunguka katika maeneo ya shule. Tulijua wanakuwa hapa kwa sababu shule iko ndani ya eneo la jeshi kwa hiyo wanakuja kuangalia usalama.
“Lakini pia zamani wanafunzi wengi walikuwa hawaingii madarasani wengi walikuwa wanajificha vichakani, tangu wamekuja hakuna wanafunzi wanaojificha.
“Hata sasa hivi unavyoona hapa hakuna wanaokuja kununua vitu hapa hadi muda uliopangwa utakapofika,” alisema mmoja wa wanawake hao.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Mbugi Nesta, alikanusha kuwapo tabia za utovu wa nidhamu wa kiasi hicho shuleni kwao na kuahidi kulifuatilia suala hilo kubaini ukweli wake.
“Mbona hakuna suala kama hilo, ila siwezi kukataa itabidi tukutane kulijadili hatujui kwa nini wamesema. Wengesema shule yetu ndiyo inayofanya vizuri katika taaluma katika ukanda huu nisingeshangaa,” alisema Mbugi.
Kuhusu kuwapo askari hao, Mbugi alisema imetokana na ahadi ya kiongozi mmoja wa jeshi alipoalikwa kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya shule hiyo ambaye aliahidi kutoa askari watakaosaidia kuhakikisha hali ya utulivu na usalama shuleni hapo.
Hata vivyo chanzo kimoja cha kuaminika kutoka ndani ya shule hiyo kiliiambia MTANZANIA kuwa wanafunzi shuleni hapo walikuwa na tabia ya ukorofi wengi wao wakishindwa kuhudhuria masomo na kujificha vichakani.
“Kuna baadhi ya wanafunzi walikuwa wanajificha wanavuta bangi na wengine walikuwa wanawakaba wenzao na wakati mwingine walikuwa wanawagomea walimu wao,” kilieleza chanzo hicho.
Pia MTANZANIA lilifika katika shule mbalimbali za msingi ikiwamo Juhudi na Vingunguti kuona hali ilivyo wakati wa mapumziko na kuwakuta watoto wengi wakinunua ice cream na vitafunwa mbalimbali vilivyokuwa vikiuzwa katika maeneo ya shule.