26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

TFDA YAIMARISHWA, MAKOSA DHIDI YAKE UHUJUMU UCHUMI

Na Shermarx Ngahemera


WAFANYABIASHARA na wananchi kwa ujumla wanaarifiwa na Mamlaka ya Dawa na Chakula Tanzania (TFDA) kuwepo kwa mabadiliko ya usimamizi ya Sheria inayounda Mamlaka hiyo kwa kuimarishwa vipengele vya Usimamizi wa Chakula, Dawa, Vipodozi na Vitendanishi kufanya makosa hayo kuwa ya uhujumu Uchumi kuanzia Julai mosi mwaka jana.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TFDA,  Hiiti Sillo, katika kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini  katika Mji wa historia wa Tabora, alisema kufuatia kuongezeka kwa madhara na tatizo la utengenezaji, usambazaji, matangazo potofu na matumizi  mabaya ya madawa duni, chakula kisichofaa kwa binadamu na vipodozi hatari kinyume cha Sheria ya TFDA Sura 219, Bunge limefanya mabadiliko na kufanya marekebisho ya  sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2016 na kuwezesha mabadiliko hayo kwa TFDA.

Mamlaka sasa inashughulikia wanaovunja sheria yake katika msingi wa uhujumu uchumi kwani makosa hayo huathiri watu wengi  na ili kulinda afya  ya Watanzania na kupunguza matukio yanayoathiri watu vibaya, imepangwa kupigwa vita vilivyo kama ufisadi.

Mwanasheria Mshauri wa TFDA, Iskari Tite, alisema makosa yanayosimamiwa na TFDA ni ya kitaifa na kimataifa na hivyo kulinda haki za kuishi (Bill of Rights) na ile ya  maisha (Right to Life), ni haki za msingi zitolewazo na Serikali kwa wananchi kulindwa dhidi ya wanaotafuta utajiri kwa nguvu kupitia mahitaji ya lazima ya binadamu.

Alisema makosa mengi kwa Mamlaka yatashughulikiwa na Mahakama ya Uhujumu Uchumi kama ufisadi  na hujuma kwa umma.

Mwanasheria huyo aliainisha kuwa mabadiliko hayo yaliyofanywa ni pamoja na makosa ya kutosajili jengo la biashara linaloshughulikia biashara na kutengeneza dawa au vipodozi kuwa ni kosa la uhujumu uchumi.

Kuuza chakula kisichofaa au kugeuza kisichofaa kitumike kwa kubadilisha tarehe au chapa, ni kosa kuhujumu uchumi na kwa makosa yote hayo adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka 15.  

Wakati huohuo kufanya matumizi ya dawa zilizopo kwenye utafiti kutumika bila kibali, adhabu  yake ni miaka mitano au faini ya Sh milioni 10.

Hivyo hivyo  dawa za miti shamba zitakuwa ni bandia na hivyo batili kama zitabadili majina na kutumia sifa ambazo hazina au hazijathibitishwa na TFDA.

Makosa mengine ni kutumia chapa zenye udanganyifu zinazodai kuwa na sifa zisizokuwepo au kuonesha kutoka ndani wakati ni bidhaa ya nje au kuhuisha vipodozi bandia kwa kuzipa tarehe zinazoonesha bado uhai wake au kutamalaki maelezo ya udanganyifu na hivyo kudanganya umma na adhabu yake ni hadi miaka 15.

Akisimulia ukubwa wa mabadiliko hayo ya sheria, Mshauri wa Sheria, Tite alisema kufuatia hali hiyo kesi za aina hiyo  ni kubwa, hazina dhamana, adhabu haipungui miaka 15 kama kikomo cha adhabu na kuwa chini ya Mahakama ya Wahujumu Uchumi badala ya Mahakama Kuu ya kawaida.

“Tunaomba vyombo vya habari vidhibiti matangazo ya dawa na chakula  kwa kudai kibali cha ithibati kutoka kwa TFDA kuwa zinasifa na uwezo unaotangazwa ili kudhibiti usahihi wa  matangazo hayo, kwani mengi yanapotosha usahihi wa mambo kwa masilahi ya  kibiashara tu na si afya ya jamii,” alisema Tite.

Akizungumzia mafanikio ya TFDA, Mkurugenzi Mkuu, Hiiti Sillo, alisema wadau wa sekta hiyo ndio waliowezesha kupata mafaniko makubwa na moyo wa uthubutu umeweza kupunguza makali ya tatizo kwa kutumia mikakati sahihi kudhibiti kupanuka kwa uhalifu huo na kutegemea uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye maabara, rasilimali watu na mtandao thabiti umefanya  TFDA wawe taasisi ongozi kwa nchi za Umoja wa Afrika Mashariki (EAC) na zile za SADC.

Anasema TFDA ni wakala wa Serikali  ulioanzishwa  chini ya kifungu na 4 (10) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 na kutumika rasmi  Julai mosi, mwaka 2003.

“Jukumu la msingi la TFDA ni kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba na vitendanishi kwa lengo la kuhakikisha kuwa bidhaa zenye usalama na ubora  unaokubalika ndizo zinazoruhusiwa kutumika nchini,” anasema Sillo.

Anasema katika ukaguzi wa bidhaa, wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza katika maeneo ya uzalishaji  na usamabazaji katika soko sanjari  na kutoa mafunzo au kufanya uhamasishaji kwa makundi tofauti ya wadau.

Uchapaji kazi

“Mamlaka  hadi sasa imetoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo  zaidi ya 300 katika mikoa mbalimbali ili kuwaelimisha masharti muhimu ya uzalishaji wa vyakula salama na bora. Inatekeleza kwa vitendo  dhana ya kufanya kazi kwa bidii au ‘hapa kazi tu’ kwa kuimarisha udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba kwani katika 2016/17 hadi Machi mwaka huu, imepokea  jumla ya maombi  mapya ya usajili wa viwanda 767 vikiwamo vya dawa kimoja, chakula 739 na vipodozi  27 ambavyo vinajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa zinazodhibitiwa na Mamlaka na hivyo kusajiliwa baada ya kukaguliwa viwanda 635.

Kati ya viwanda hivyo, 613 ni vya vyakula, dawa kimoja na vipodozi 21, ikiwa ni asilimia 82.8 ya maombi yote na hivyo kuashiria viwanda vingi kuzingatia sheria na kuzalisha bidhaa salama.

Anasema katika kipindi hicho hicho, kilifanya tathmini ya maombi 4762 ikiwa  ni asilimia 82.1 ya usajili wa bidhaa za dawa na chakula, vifaa tiba, vipodozi.  Kati ya maombi 5802 yaliyowasilishwa ni 4322 yaliidhinishwa, ikiwa ni asilimia 75  na maombi 441 yalikataliwa na  ikiwa ni asilimia 25 kwa kukosa vigezo vya ubora na usalama.

Kutokana na kuwekeza vilivyo katika maabara, Mamlaka imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya na kujiridhisha kuhusu taarifa za kisayansi juu ya uzalishaji wa bidhaa husika kabla ya kufanya maamuzi ya usajili au kuendelea kutumika; hivyo jumla ya sampuli 8066 kati ya sampuli 8093 za bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba zilichunguzwa ambapo sampuli 6697 sawa na asilimia 83 zilifaulu na sampuli 347 hazikukidhi vigezo na hivyo asilimia 17 kutosajiliwa au kutolewa kwenye soko.

Mkurugenzi Mkuu Sillo alibainisha kuwa Mamlaka ilikamata na kuteketeza bidhaa tani 631.7 zenye thamani ya Sh 797,312,103.15  zisizofaa zikiwa tani 407.3 zenye thamani ya Sh 601 ,301,867.9 zilitolewa taarifa kwa hiari na tani 134.4 zenye thamani ya Sh 196,010,235.25  zilikamatwa katika kaguzi mbalimbali.

Kubadilika mbinu za uhalifu

Mamlaka imebaini kuwa mbinu na mwenendo wa usafirishaji wa magendo ya bidhaa na wahalifu kwa kutumia vifaa visivyotiliwa shaka lakini raia wema wamekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa na mizigo hiyo kukamatwa.

Mbinu hizo ni pamoja na kutumia matanki na matenka ya mafuta kutoka Kenya na  DR Congo kwenye maghala ya wafanyabiashara Kariakoo ambapo jumla ya tani 70.56  za bidhaa mchanganyiko nchini kote zenye thamani ya Sh milioni 649.9 na bidhaa ziliteketezwa vilivyo.

Kuanzia Julai mwaka 2015 hadi Machi mwaka huu, walimu na wanafunzi 64,479 walipewa  elimu katika mikoa 11 ikiwamo ya Ruvuma, Lindi, Pwani, Mwanza, Shinyanga, Geita, Mbeya, Rukwa, Tanga, Simiyu na Songwe ili kupanua wigo wa uelewa kuhusu shughuli za TFDA katika kulinda afya ya jamii.

“Inafurahisha kuwaarifu kuwa TFDA imefanikiwa kitaasisi kuwa kiongozi wa taasisi zote za aina yake Afrika Mashariki na SADC na kufanya taarifa na maabara zake kuwa zenye ithibati ya kimataifa na kuaminika kwa umahiri wa taarifa zake,” alisema Mkurugenzi Sillo.

Anasema maabara ya kisasa ya ISO 17025 ya kitaifa na kimataifa ya vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO)  itazinduliwa karibuni jijini Mwanza, kuhudumia kwa karibu mikoa ya kanda ya ziwa na  kupunguza kazi kwa ile ya Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

Changamoto kubwa kwa TFDA inatokana na ukweli kuwa nchi zote zinazoizunguka Tanzania ni uchumi huria na hazina sheria mahiri ya katazo kuhusu sekta hii.

Kwa nchi hizo kujali sana faida ya kiuchumi zaidi kuliko masilahi mapana ya wananchi wake na kufanya suala la udhibiti kuwa gumu kutokana na mwingiliano mkubwa wa nchi hizo na Tanzania kwenye dawa, chakula, na vipodozi bila mwongozo wa maana.

TFDA imeimarisha mifumo yake ya elektroniki na hivyo kuweza kufuatilia kwa karibu mwenendo wa utoaji taarifa za madhara  mabaya (Adverse drugs reactions- ADR) kwa matumizi ya bidhaa za dawa, vipodozi na chakula na bidhaa zinazozidhibitiwa na Mamlaka kwa kutumia simu.

Hadi sasa idadi ya malalamiko imefikia 71 ikiwa ni asilimia 44 ya taarifa zote toka  Oktoba mwaka jana.

Kuhusu wajasiriamali kulalamikia gharama kubwa za vipimo na leseni, Mkurugenzi Sillo amekanusha hali hiyo na kusema viwango vyao ni shindani na vya chini ukifananisha na vile vya Marekani na Afrika Kusini kwa ukaguzi wa makazi na dawa na gharama za leseni,  kwani TFDA hutoza dola 6,000 kila moja, Marekani ni dola 190,000  wakati  Afrika Kusini ni dola 20,000. Kwenye ukaguzi dawa TFDA   gharama zake ni dola 6,000 ukifananisha  na dola 300,000 Marekani na Dola 10,000 Afrika Kusini.

“PMS ni programu ya TFDA ya kupambana na dawa duni ambazo zimekithiri ulimwenguni,” alisema.

 

DONDOO

  1. Huduma za maabara ni muhimu  kwa mdhibiti ili kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kile anachofanya- Agnes Kijo Meneja Usajili wa vifaa Tiba na vitendanishi
  2. Soko la dawa duniani lina thamani ya dola bilioni 500 na dawa bandia ni asilimia 10 wakati Tanzania na nchi ya Kusini ya Jangwa la Sahara ni asilimia 25 hadi 30 dawa bandia au duni  -Dr Edgar Mahundi Meneja TFDA wa Zoni ya Magharibi.
  3.  Tatizo la Mkoa wa Tabora ni ushirikina na imani potofu – Aggrey Mwanri Mkuu wa Mkoa Tabora
  4. Dawa duni zisiruhusiwe kuuzwa nchini – Aggrey Mwanri Mkuu Mkoa Tabora
  5. Ni kosa la uhujumu uchumi kuuza chakula kisichofaa kwa binadamu – Hiiti Sillo

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles