26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TET, DIT kuandika vitabu vya ufundi shule za Sekondari

Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa uandishi wa vitabu 32 vya kiada vya masomo nane ya ufundi kuanzia Kidato cha kwanza hadi cha nne.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Aneth Komba na Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Profesa Preksedis Ndomba wakisaini makubaliano ya uandishi wa vitabu 32 vya kiada vya masomo ya ufundi shule za Sekondari nchini.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Juni 17, 2021 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo amesema ni wazi kuwa wataalamu wa masomo ya ufundi wapo kwenye vyuo vya ufundi na hana shaka na wataalamu waliobobea na wenye weledi kutoka DIT ambapo inategemewa kupatikana kwa kazi nzuri na yenye viwango stahiki.

“Nipongeze sana hili na nina imani kuwa tutapata vitabu bora vitakavyosaidia ujifunzaji na ufundishaji na mwisho kupatikana kwa wahitimu mahiri wenye ujuzi katika fani mbalimbali za Ufundi.

“Kazi ya uandishi wa vitabu ni kazi inayohitaji umakini wa hali ya juu, hivyo nasisitiza umakini katika kazi hii ili kuhakikisha kuwa tunapata vitabu ambavyo ni bora. Aidha, nisisitize kuwa, ushirikiano huu ambao viongozi wa taasisi hizi mbili za elimu zinatiliana saini leo, utaendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya kila Taasisi. Kupitia ushirikiano huu, kila taasisi itakuwa na jambo la kujifunza kutoka kwa mwenzake. Naomba mjifunze yale mazuri na kuyaendeleza,” amesema Dk. Akwilapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba amesema vitabu hivyo vimeandikwa kwa kutumia mihtasari iliyoboreshwa ya mwaka 2019.

Amesema vitabu hivyo ni vya masomo yote nane ya shule za ufundi kama yalivyoainishwa na serikali na kwamba kwa sasa Taasisi ya Elimu haina wataalamu wa masomo hayo.

“Hivyo kwa kuzingatia kwamba vitabu hivyo ni nyenzo muhimu ya kufundishia na kujifunzia na kwa kuwa DIT ina wataalamu watakaoweza kuratibu zoezi hilo la uandishi wa vitabu hivyo, TET ilifanya mazungumzo na DIT na kufikia makubaliano yatakayoanza utekelezaji Juni 22, mwaka huu na kukamilika ndani ya siku 160,” amesema Dk. Aneth.

Pamoja na mambo mengine, Dk. Aneth amesema anatarajia baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, DIT inashirikiana na vyuo vingine vya ufundi kutoa mafunzo kwa walimu kazini ili waweze kutekeleza mtaala kwa kadiri ya matarajio.

“Tunawashukuru sana wenzetu wa DIT na menejimenti yake kwa kukubali ombi letu la kuratibu kuandika vitabu hivi na TET, ni matumaini yangu tutapata vitabu bora hasa ukizingatia vinaandikwa na wataalamu wanaofundisha masomo ya ufundi,” amesema Dk. Aneth.

Naye Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba ameishukuru TET kwa kuiamini DIT kufanya kazi hiyo huku akiwahakikishia kazi hiyo itafanyika kwa weledi wa hali ya juu kwani inaendana na dira ya taasisi hiyo.

“Kwa pamoja tuna jukumu la kuhakikisha tunamaliza kazi hii kwa wakati na imetupa hamasa kwamba serikali iko pamoja na sisi ndiyo maana tulipoombwa na TET tulikubali mara moja kwa sababu inaendana na dira yetu ya kutatua changamoto katika jamii,” amesema Profesa Ndomba.

Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Dk. Richard Masika amewatoa hofu na kuwahakikishia TET kuwa DIT ina wataalamu wa kutosha na wenye weledi mkubwa na kwamba kazi hiyo itafanyika kwa umakini mkubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles